
……
Cannes, Ufaransa
Katika kuendeleza jitihada za kukuza diplomasia ya utamaduni na kuifungua sekta ya filamu ya Tanzania kwa masoko ya kimataifa, Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Mheshimiwa Saidi Yakubu, amekutana na viongozi wa Tamasha la Filamu la Cannes kwa mazungumzo yaliyolenga kuimarisha ushiriki wa Tanzania katika tamasha hilo maarufu duniani pamoja na kutafuta fursa za ushirikiano kwa wadau wa sekta ya filamu nchini.
Katika kikao hicho, Mheshimiwa Balozi alikutana na Bw. François Desrousseaux, Afisa Mwandamizi anayehusika na mahusiano ya kimataifa na ushirikiano wa kimkakati katika Tamasha la Filamu la Cannes, ambaye amekuwa akishiriki katika kuratibu ushiriki wa nchi mbalimbali, taasisi za filamu na wadau wa kimataifa katika shughuli za tamasha hilo. Aidha, alikutana na Bw. Guillaume Esmiol, Mkurugenzi Mtendaji wa Marché du Film (Soko la Filamu la Cannes), ambalo ni jukwaa kubwa zaidi duniani la biashara ya filamu, linalowakutanisha wazalishaji, wasambazaji, wawekezaji, majukwaa ya utiririshaji (streaming platforms), studio na wabunifu wa maudhui kutoka zaidi ya nchi 140 kila mwaka.
Mheshimiwa Balozi aliambatana na Bw. Jigar Ganatra, mtayarishaji na mwongozaji wa filamu kutoka Tanzania mwenye uzoefu mkubwa wa kimataifa katika utengenezaji wa filamu na vipindi vya televisheni vya mazingira, wanyamapori na maudhui ya ukweli (factual productions). Kupitia kazi zake, Bw. Ganatra ameshiriki uzalishaji wa maudhui katika zaidi ya nchi 26 duniani, akitangaza urithi wa asili, utalii na uhifadhi wa mazingira kwa hadhira ya kimataifa.
Mazungumzo hayo yalijikita katika namna Tanzania inaweza kuongeza ushiriki wake katika Tamasha la Filamu la Cannes kuanzia mwaka 2027, ikiwemo uwepo wa banda la Tanzania, ushiriki wa watayarishaji na waigizaji wa Kitanzania, fursa za mafunzo kwa vijana, ushirikiano katika uzalishaji wa filamu za kimataifa (co-productions), upatikanaji wa masoko ya kimataifa pamoja na kuitangaza Tanzania kama kitovu cha utengenezaji wa filamu na maudhui ya ubunifu barani Afrika.
Akizungumza baada ya kikao hicho, Mheshimiwa Saidi Yakubu alisema kuwa sekta ya filamu ni moja ya maeneo yenye uwezo mkubwa wa kuchangia ukuaji wa uchumi, ajira kwa vijana, utalii na utangazaji wa taswira ya Tanzania duniani. Alieleza kuwa Ubalozi utaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa Ufaransa na Ulaya ili kufungua milango ya ushirikiano, uwekezaji na masoko mapya kwa wabunifu na watayarishaji wa maudhui kutoka Tanzania.
Aliongeza kuwa ushiriki mkubwa wa Tanzania katika majukwaa ya kimataifa kama Tamasha la Filamu la Cannes utawezesha hadithi za Tanzania kufikia hadhira pana zaidi duniani, huku ukiimarisha nafasi ya nchi katika uchumi wa ubunifu unaokua kwa kasi duniani.
Kikao hicho ni sehemu ya mkakati mpana wa Ubalozi wa Tanzania nchini Ufaransa wa kutumia diplomasia ya utamaduni na ubunifu kama nyenzo za kuimarisha mahusiano ya kimataifa, kuvutia uwekezaji na kuendeleza ukuaji wa sekta za filamu, sanaa na utalii nchini Tanzania.
