Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira akiwahutubia mamia ya wana CCM na wananchi wa Kigoma mjini leo Mei 16, 2026 katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Kawawa uliopo Kigoma mjini akiwa katika siku yamwisho ya ziara yake ya siku tatu mkoani humo.

………

Asema ni kabla ya kuanza kwa mchakato maridhiano kisiasa,waliohusika wabainishwe

*Ampongeza Rais Samia kuunda Tume kuchunguza kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu

*Aweka wazi kuwa na vyama vingi isiwe sababu kuanzisha vurugu,kuvunja amani iliyopo nchini

Na MWANDISHI WETU

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira amesema kabla ya kuanza kwa mchakato wa maridhiano ya kisiasa, ni vyema kuwabaini na kuwachukulia hatua za kisheria kupitia vyombo vya haki watu waliohusika na vurugu zilizosababisha madhara vikiwamo vifo.

Amempongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuunda Tume ya Kuchunguza Vurugu za Wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 kwa lengo la kujua kiini cha tatizo hilo.

Wasira alieleza hayo mwishoni mwa wiki alipohutubia mkutano wa hadhara uliofanyika Mjini Kigoma mkoani Kigoma akiwa katika ziara ya kichama katika mkoa huo.

“Sijasema jina la mtu, lakini wenye kujua hayo mambo wanajijua, waache jinai ichunguzwe kama walihusika waende kwenye vyombo vya haki na sio wengi, wanaobaki watu wema tukae tufanye nao maridhiano,” alisema.

Wasira pia alimpongeza Rais Dk.Samia kwa kuunda tume ya kusaidia kujua chanzo cha vurugu hizo huku akitumia nafasi hiyo kuipongeza kazi nzuri iliyofanywa na tume hiyo kufanya uchunguzi huo.

“Rais (Dk. Samia) tunamshukuru na kumpongeza sana, kwa kuunda tume ya kutusaidia kujua chanzo. Tunampongeza na tunaipongeza tume ambayo imesema katika uchunguzi wake imegundua kuna watu si wengi lakini ndio walioanza mpango ule walifadhili.

“Sasa wanasema (tume) wao hawakuwa polisi wa kuwakamata, lakini wanasema tuchunguze wale walioonekana ili tusiwe tunafuga nyoka ndani ya nyumba,” alisema na kuongeza hakuna anayeshabikia matukio yenye kuumiza yaliyosababisha vifo na kwamba anayefanya hivyo hayuko sawa kiakili.

Aliongeza “Wanasema watu wamekufa, ni nani anafurahia kufa watu labda uwe na wewe akili yako imeharibika kama unasherehekea kufa watu. Wote tunapinga mauaji, lakini nani amesababisha, halafu wale walioko wengine kama tunawahisihisi ndio tena wanataka kutufundisha namna ya kufanya…vurugu muanzishe nyie na namna ya kumaliza mgogoro mtupe nyie, hapana.”

Kwa mujibu wa Wasira pamoja na kutofautiana kimawazo huenda wapo watu wema ambao wanaweza kukaa meza moja na kujadiliana mustakbali mwema.

“Mnaweza kuwa mnatofautiana mawazo lakini ni watu wema tu, kutofautiana mawazo si mbaya ni jambo la kawaid tu, hamuwezi kusema wote mtakuwa mnakubaliana, hata kondoo hawakubaliani mwengine anatangulia mbele mwengine nyuma.Hivyo wengi wanakubaliana maridhiano yafanyike baada ya waovu kupatikana,” alieleza.

VYAMA VINGI SIO UHASAMA

Katika hatua nyingine Majamu Mwenyekiti Wasira alisema Watanzania walikubaliana kuingia katika mfumo wa vyama na usiwe chanzo cha vurugu.

“Viko vyama vingi na tulikubaliana viwepo lakini hatukukubaliana mfumo wa vyama vingi uwe chanzo cha mgogoro katika nchi yetu, kama wewe una chama na unadhani amani si kitu cha maana umekosea, sisi tunataka amani,” alisisitiza.

 

Alifafanua mkoa wa Kigoma ni shuhuda wa madhara ya kutoweka amani kwa kuwa umewahi kupokea wakimbizi waliozikimbia nchi zao kutokana na machafuko.

 

“Sisi wa Kigoma si watu wa kufundishwa gharama ya amani, nyinyi mmeishi mahali ambapo amani hakuna, nyinyi mmekuwa wenyeji wa watu waliokimbia fujo wameishi hapa na kuwatoa hapa ikawa shughuli, maana wanaona sasa amani hii tuiache tumuachie nani mpaka ikabidi kushauriana nao.

“Nchi zote zinazozunguka hapa zimewahi kuleta wakimbizi Kigoma, sasa nyinyi mnataka fujo mtakimbilia wapi, mnaijua safari ya sisimizi huwa wanaenda na huku wanarudi sasa haijulikani wanakokwenda…sisi hapa tumepokea wakimbizi kwa maelfu sasa watu wanavuruga amani eti wanasema kuvuruga amani ndilo jibu la haki…” alikumbusha Wasira.