Mbunge wa Viti Maalum anayewakilisha kundi la watu wenye ulemavu Nassirya Ally amesisitiza umuhimu wa jamii kujifunza na kutumia lugha ya alama ili kujenga taifa lenye usawa na ujumuishi kwa watu wote bila ubaguzi.

Mbunge huyo ametoa kauli hiyo wakati alipohudhuria kongamano pamoja na mahafali ya mwaka wa tatu ya wahitimu wa Lugha ya Alama yaliyoandaliwa na Jumuiya ya Lugha ya Alama ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOSLA) yaliyofanyika katika ukumbi wa Theatre Two, CoED – UDOM.Akizungumza katika kongamano hilo, Nassirya amesema matumizi ya lugha ya alama ni nyenzo muhimu ya kuwaunganisha watu wenye ulemavu wa kusikia na jamii inayowazunguka, huku akieleza kuwa elimu ya lugha hiyo inapaswa kupewa nafasi kubwa katika taasisi mbalimbali ili kuondoa vikwazo vya mawasiliano.

“Jamii inapaswa kuelewa kuwa lugha ya alama si kwa watu wenye ulemavu wa kusikia pekee, bali ni daraja la mawasiliano linalojenga heshima, usawa na ujumuishi katika jamii yetu,” amesema Nassirya.

Pia Nassirya amewahimiza wadau mbalimbali kushirikiana katika kuhamasisha matumizi ya Lugha ya Alama ya Kitanzania ili kuhakikisha watu wenye mahitaji maalum wanapata haki sawa katika huduma za kijamii, elimu na ajira.Katika hafla hiyo, risala maalum iliyosomwa mbele ya mgeni rasmi ambapo Jumuiya ya UDOSLA ilieleza historia ya Taasisi hiyo iliyoanza mwaka 2021 ikiwa na wanafunzi wanane pekee kabla ya kusajiliwa rasmi mwaka 2025. Risala hiyo pia ilibainisha mafanikio mbalimbali yaliyofikiwa ikiwemo ongezeko la wanachama zaidi ya 150 na kuhitimu kwa wahandisi wa mawasiliano zaidi ya 50 wenye ujuzi wa Lugha ya Alama.

Aidha, kupitia risala hiyo, jumuiya hiyo ilieleza changamoto zinazowakabili wahitimu wa Lugha ya Alama ikiwemo ukosefu wa ajira rasmi, uhaba wa vifaa vya kufundishia pamoja na uhitaji wa miundombinu bora ya kujifunzia.