NA: MWANDISHI WETU, PANGANI

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Funguni ya wilayani Pangani mkoani Tanga wamefundwa masuala mbalimbali yahusuyo elimu, maadili, ukatili wa kijinsia na utunzaji mazingira na viongozi wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kilele cha Juma la Wazazi ambapo kiwilaya yamefanyika shuleni hapo.

Elimu hiyo imetolewa Mei 16, 2026, na viongozi na wajumbe wa Jumuiya hiyo katika kuhakikisha wanafunzi hao wanafanya vizuri katika masomo yao na kuwajenga katika maadili mazuri ili kujenga jamii yenye maadili na maendeleo.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wilaya na Mjumbe wa Kamati ya Siasa, Waziri Mbezi amewasisitiza wanafunzi kusoma kwa bidii ili waweze kutimiza ndoto zao za kimaisha kwani elimu ndiyo uwekezaji bora.

“Wanafunzi niwasisitize kufanya bidii sana katika kusoma, maisha yamebadikika, zamani maisha yalikuwa rahisi sana hata bila kusoma mtu ungeweza kuishi, lakini sasa hivi maisha yamebadikika, kila kazi inahitaji mtu aliyesoma”.

Vilevile, Mbezi amesema serikali imewekeza fedha nyingi katika elimu kutokana na umuhimu wake, hivyo ni vyema kuongeza bidii ili uwekezaji huo ulete tija iliyotarajiwa katika kuchochea maendeleo ya Taifa.

Katika hatua nyingine, Katibu Muhtasi Ofisi ya Mbunge na Mjumbe wa Kamati ya Siasa wilaya, Aisha Msofe, amepongeza ubunifu wa walimu wa shule hiyo kwa kuwafundisha ujasiriamali wanafunzi hao kwa vitendo.

“Nimeona ubunifu wenu walimu wa kuwafundisha vijana ujasiriamali, hii nimependa sana kwani itawasaidia katika maisha yao kwa kujipatia kipato,” amesema Msofe.

Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji Jumuiya hiyo wilaya, Ramadhani Mohamed (Molinga) amewaasa wanafunzi hao kuwalipa wema wazazi wao wanaopambana kuwapatia mahitaji muhimu kwa kuhakikisha wanasoma kwa bidii ili wafanye vizuri katika masomo yao.

Wajumbe wengine wamewashauri wanafunzi kuwa na nidhamu kwani nidhamu ni msingi wa mafanikio. Aidha, wamesisitizwa kuheshimu wazazi na walimu wao, kuacha kujihusisha na mapenzi, makundirika mabaya na kuepuka kuingia katika kumbi za starehe.

JMUIYA YAACHA NEEMA FUNGUNI SEKONDARI

Katika maadhimisho hayo, Jumuiya hiyo imeahidi kutoa shamba lililoko Mtaa wa Boza ili litumike kwa ajili ya uzalishaji wa chakula cha wanafunzi shuleni ili wanafunzi wapate chakula wawapo shuleni.

Vilevile, Jumuiya imeahidi kutoa zawadi ya shilingi 100,000 kwa mwanafunzi atakayepata ufaulu wa Daraja la Kwanza katika Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne na shilingi 50,000 kwa wanafunzi wa Kidato cha Pili.

Pia, Jumuiya imeahidi kuchangia mchele kilo mia moja katika Mahafali ya Kidato cha Nne mwaka huu kutokana na shule hiyo kufanya vizuri kitaaluma ndani ya wilaya.

Jumuiya pia imeshiriki kufanya usafi wa mazingira na kupanda miti shuleni hapo ikiwa ni juhudi za kuhifadhi mazingira.

Mkuu wa Shule hiyo, Nassoro Gamba ameishukuru Jumuiya hiyo kwa kuchagua kufanya maadhimisho shuleni kwake. Pia, ameshukuru elimu nzuri iliyotolewa ya ukatili wa kijinsia, utunzaji mazingira na maadili kwani itawasaidia wanafunzi hao kuwajenga kimaadili na kuwa raia wema.