Na Prisca Libaga,  Arusha
RC  Makalla akaribisha watalii na wawekezaji kutoka Urusi kuwekeza katika sekta ya utalii
– Wapendekeza ushirikiano wa Mkoa wa Arusha na Mkoa mmoja wa Urusi
-Waziri Reshetnikov avutiwa na  ukarimu wa watanzania, Amani na utunzaji wa vivutio vya utalii
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla leo Jumamosi Mei 16, 2026 amekutana na kufanya mazungumzo na Ujumbe wa Serikali ya Shirikisho la Urusi ulioongozwa na Waziri wa maendeleo ya uchumi Mhe. Maxim Gennadyevich Reshetnikov akiwakaribisha watalii na wawekezaji kutoka Nchini Urusi kuja kutalii na kuwekeza katika sekta ya utalii Mkoani Arusha.
Katika mazungumzo ya Viongozi hao yaliyofanyika kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Jijini Arusha, Viongozi hao pia wamejadiliana na kupendekeza ushirikiano wa Mkoa wa Arusha na Mkoa mmoja wa Urusi ili kushirikiana katika sekta mbalimbali za maendeleo pamoja na kubadilishana uzoefu ili kunufaisha pande hizo mbili kwa maslahi ya maendeleo na ustawi wa wananchi wa Mkoa wa Arusha na Mkoa utakaochaguliwa kutoka Nchini Urusi.
Kwa upande wake Mhe. Reshetnikov amemshukuru Mhe. Makalla kwaniaba ya serikali ya Tanzania kwa mapokezi mazuri aliyoyapata na ujumbe wake tangu alipofika Mkoani Arusha jana Mei 15, 2026, akionesha pia kuvutiwa na ukarimu wa Watanzania, amani iliyopo Nchini pamoja na utunzaji mkubwa wa Vivutio vya utalii vilivyopo Mkoani Arusha.
Katika kikao hicho Mhe. Makalla ameshiriki pamoja na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na uwekezaji Mhe. Dkt. Pius Stephen Chaya, Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha Dkt. Toba Alnason Nguvila na Maaafisa wa taasisi za serikali zilizopo Mkoani Arusha huku upande wa Waziri Reshetnikov akiambatana na Balozi wa Urusi Nchini Tanzania Mhe. Andrey Avetisyan na Maafisa wengine kutoka serikali ya Urusi, Mhe. Reshetnikov akitembelea na kutalii pia kwenye hifadhi ya Taifa ya Arusha jana Ijumaa akiambatana na ujumbe wake.