Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb) akijibu swali la Mbunge wa Ilemela Mhe. Kafiti William Kafiti, aliyetaka kujua ni lini Serikali itaandaa Kanuni za Bima za lazima ili kutekeleza Sheria ya Fedha ya Mwaka 2022 na kuongeza Mapato ya Serikali, bungeni jijini Dodoma.
Na Peter Haule, WF, Dodoma
Serikali inaendelea na zoezi la ukusanyaji wa maoni kutoka kwa wadau mbalimbali kuhusu rasimu ya Kanuni za bima za lazima baada ya kukamilisha maandalizi ya rasimu ya Kanuni za bima hizo.
Hayo yamebainishwa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Ilemela Mhe. Kafiti William Kafiti, aliyetaka kujua ni lini Serikali itaandaa Kanuni za Bima za lazima ili kutekeleza Sheria ya Fedha ya Mwaka 2022 na kuongeza Mapato ya Serikali.
Mhe. Munde alisema kuwa Serikali, kupitia Sheria ya Fedha Namba 5 ya mwaka 2022, ilifanya marekebisho ya Sheria ya Bima Sura 394 ili kuongeza wigo wa bima za lazima kwa lengo la kuongeza kinga kwa majanga ambayo yana madhara makubwa kwa wananchi yanapotokea.
Alisema kuwa utekelezaji wa marekebisho hayo katika Sheria husika unailazimu Serikali kuandaa Kanuni, aidha kwa kuzingatia umuhimu wa suala hili alieleza kuwa Serikali imedhamiria kukamilisha mchakato huo mapema iwezekanavyo.
