Na John Bukuku, Dar es Salaam

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Serikali pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imefanikiwa kukamata jumla ya lita 66,048 za kemikali bashirifu katika operesheni maalum iliyofanyika jijini Dar es Salaam mwezi Aprili mwaka huu.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika  jijini Dar es Salaam Kamishna wa mamlaka hiyo Aretas James Lyimo amesema kemikali zilizokamatwa ni Cyclohexanone zenye ujazo wa lita 16,048 pamoja na Extra Neutral Alcohol (ENA) zenye ujazo wa lita 50,000 ambazo zilikuwa zikiingizwa na kusafirishwa kinyume na taratibu za kisheria.

Amesema magari mawili yaliyokuwa yakitumika kusafirisha kemikali hizo yameshikiliwa huku watuhumiwa wawili wakikamatwa kuhusiana na tukio hilo. Aidha, uchunguzi wa awali umebaini kuwa kemikali aina ya Cyclohexanone ziliingizwa nchini na kampuni ya Kinglion Investment Company LTD bila kufuata matakwa ya mifumo ya udhibiti ikiwemo kukosa vibali kutoka mamlaka husika.

“Kutokana na udhibiti wa dawa za kulevya kuimarika duniani, mitandao ya kihalifu imekuwa ikitumia kemikali bashirifu kuzalisha dawa za kulevya katika maabara bubu. Kemikali hizo hutumika kihalali katika sekta mbalimbali ikiwemo viwandani, kitabibu, kilimo, ujenzi, madini pamoja na tafiti za kisayansi, lakini wahalifu huzichepusha na kuzitumia kutengeneza dawa za kulevya,” amesema.

Ameongeza kuwa kemikali aina ya Extra Neutral Alcohol (ENA) zilikuwa zinasafirishwa kwa kutumia magari ya kubeba mafuta ya petroli yenye alama ya “Danger Petroleum 3YE 1203” kwa kutumia vibali vya kughushi, huku magari hayo yakidaiwa kubeba kemikali hizo kutoka kampuni ya Maranile Group Company Limited.

Katika operesheni hiyo, mamlaka ilimkamata Bakira Abel Zacharia (44), mkazi wa Dar es Salaam, dereva wa gari namba T 794 BMB lenye tela tanki namba T 166 AHW lililokuwa limebeba lita 30,000 za kemikali hizo. Pia, alikamatwa Vicent Stephen Rashid (26), mkazi wa Mbeya, dereva wa gari namba T 568 EQF lenye tela tanki namba T 640 EQN lililokuwa limebeba lita 20,000 za kemikali hizo.

“Mazingira ya uingizaji na usafirishaji wa kemikali hizo yanaashiria uwepo wa nia ovu ya kuzichepusha kwa matumizi haramu ikiwemo utengenezaji wa dawa za kulevya. Kemikali aina ya Cyclohexanone ni miongoni mwa kemikali zilizothibitika kimataifa kutumika katika maabara bubu zinazozalisha dawa za kulevya aina ya Phencyclidine (PCP),” amesema.

Aidha, amesisitiza kuwa lita 16,048 za kemikali aina ya Cyclohexanone zilizokamatwa kama zingechepushwa, zingeweza kuzalisha tani 11.4 za dawa za kulevya aina ya Phencyclidine kutokana na uwezo wa kilo moja ya kemikali hiyo kuzalisha takribani gramu 750 za dawa hizo.

Kwa mujibu wa mamlaka hiyo, Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali za Viwandani na Majumbani Sura ya 182 inahitaji taratibu maalumu za usafirishaji wa kemikali ikiwemo vibali vya kuingiza na kusafirisha kemikali.
“Matumizi ya vibali vya kughushi pamoja na utoaji wa taarifa za uongo kuhusu matumizi yaliyokusudiwa ya kemikali husika ni kosa la jinai. Usafirishaji wa kemikali kwa njia fiche hususan kwa kutumia magari ya kubeba petroli ni ukiukwaji mkubwa wa taratibu za udhibiti wa kemikali,” amesema.

Sambamba na operesheni hiyo, mamlaka ilifanya operesheni nyingine katika mikoa ya Dodoma, Mtwara, Njombe, Ruvuma, Kilimanjaro, Arusha, Dar es Salaam, Morogoro na Mwanza ambapo jumla ya tani 5.733 za bangi, tani 1.67 za mirungi, gramu 48.23 za heroin pamoja na gramu 113.35 za cocaine zilikamatwa.
Aidha, ekari 38.5 za mashamba ya bangi ziliteketezwa huku magari manne pamoja na pikipiki 14 zilizohusishwa na biashara hiyo haramu zikikamatwa. Jumla ya watuhumiwa 84 walikamatwa kuhusiana na operesheni hizo.

Mamlaka hiyo imesisitiza kuwa itaendelea kushirikiana na taasisi za kitaifa na kimataifa kuimarisha udhibiti wa kemikali bashirifu zinazoweza kutumika katika utengenezaji wa dawa za kulevya.

Pia imewataka wadau wa kemikali kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa pamoja na kutoa ushirikiano kwa vyombo vya udhibiti ili kulinda usalama wa jamii na uchumi wa nchi. Wananchi wamehimizwa kuendelea kutoa taarifa za vitendo vinavyohusiana na dawa za kulevya pamoja na uchepushaji wa kemikali bashirifu ili kusaidia juhudi za Serikali katika mapambano dhidi ya biashara na matumizi ya dawa za kulevya.