Benki ya Dunia (WB) imeipongeza Serikali katika huduma ya maji kwa wananchi.

Pongezi hizo zimeelekezwa jijiji Dodoma kwa Wizara ya Maji kwa kuwa kinara wa kuigwa barani Afrika katika utekelezaji wa miradi ya maji vijijini kupitia mfumo wa malipo kwa matokeo (P4R) katika kikao kilichowakutanisha Menejimenti ya Wizara ya Maji na ujumbe kutoka WB.

Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi wa Kanda wa Benki ya Dunia Mashariki na Kusini mwa Afrika, Bi. Anna Wellenstein amesema Tanzania imefanikiwa kutekeleza kwa ufanisi miradi mbalimbali ya maji vijijini inayofadhiliwa na WB kupitia mfumo wa P4R, hatua ambayo imeonesha mafanikio makubwa katika utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mtandao wa Taifa wa Usambazaji Maji.

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuweka mazingira mazuri ya ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa maendeleo, hali inayowezesha utekelezaji wa miradi ya maji nchini.

Waziri Aweso ameielekeza Menejimenti ya Wizara ya Maji kuendelea kuimarisha ushirikiano na WB ili kuhakikisha miradi yote ya maji inakamilika kwa wakati na kuendelea kusogeza mbele azma ya Serikali ya kuhakikisha vijiji vyote nchini vinapata huduma ya maji safi na salama ifikapo mwaka 2030.

Kikao hicho pia kilijadili mafanikio ya ushirikiano kati ya Wizara ya Maji na WB pamoja na vipaumbele vya hatua inayofuata katika maendeleo ya Sekta ya Maji kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Ujumbe wa Benki ya Dunia uliambatana na Bi. Soma Ghosh Moulik, Meneja wa Sekta ya Maji, Bi. Zhimin Mao, Mtaalamu wa Rasilimali za Maji, Bw. Ernest Ruzindaza, Mchumi Mkuu pamoja na Luth Kennedy-Walker, Mratibu wa Miradi ya Benki ya Dunia.