MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi ,akiwahutubia Viongozi na Wanachama mbalimbali wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja katika mwendelezo wa ziara yake ya kuimarisha Chama Cha Mapinduzi katika ukumbi wa Dk.Mohamed Shein uliopo Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja.

NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa,akitoa salamu za Chama Cha Mapinduzi katika mwendelezo wa ziara ya Makamu Mwenyekiti ya kuimarisha Chama Cha Mapinduzi katika ukumbi wa Dk.Mohamed Shein uliopo Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja.

BAADHI ya Viongozi na Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi wakifuatilia hotuba ya Makamu Mwenyekiti katika mwendelezo wa ziara yake ya kuimarisha Chama Cha Mapinduzi katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) wa Dk.Mohamed Shein uliopo Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja.

…….

NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR

MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amewasihi viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa mstari wa mbele katika kuwaunganisha wanachama na kuimarisha mshikamano ndani ya chama.

Dk. Mwinyi amesema baadhi ya viongozi wakiwemo wabunge, wawakilishi na madiwani wamekuwa wakijihusisha na makundi yasiyofaa kwa ajili ya kulinda maslahi yao ya kisiasa, jambo ambalo linaweza kuhatarisha uimara na umoja wa CCM.

Amesema hayo katika mwendelezo wa ziara yake ya kuimarisha chama, iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) wa Dk. Mohamed Shein, Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja.

Alifafanua kuwa kuwepo kwa makundi ya kumuunga mkono mgombea wakati wa uchaguzi ni jambo la kawaida kisiasa, lakini baada ya uchaguzi kukamilika na viongozi kupatikana, makundi hayo yanapaswa kuvunjwa na wanachama wote kubaki wamoja chini ya uongozi uliopo madarakani.

“Viongozi wa CCM wanapaswa kuwa mfano wa kuunganisha wanachama badala ya kuendeleza migawanyiko isiyo na tija kwa chama,” alisema Dk. Mwinyi.

Aidha, alisema si utamaduni wa CCM kwa baadhi ya viongozi kutoa zawadi au misaada kwa wanachama wachache wanaowaunga mkono huku wakiwatenga wengine, hali ambayo husababisha malalamiko na migogoro isiyo ya lazima ndani ya chama.

“Ndugu viongozi wa Chama chetu cha Mapinduzi, ili chama kiendelee kuwa imara kisiasa na kiuchumi ni lazima tupinge kwa nguvu zote makundi yasiyofaa na tuendelee kuwa wamoja,” alisisitiza Dk. Mwinyi.

Akizungumzia ziara hiyo, alisema lengo lake ni kuwapongeza viongozi na wanachama wa CCM kwa ushindi mkubwa walioupata katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Dk. Mwinyi alisema CCM inapaswa kuendelea kuimarisha uchumi wake kwa kuvutia wawekezaji wenye uwezo wa kuanzisha miradi mikubwa ya maendeleo, akieleza kuwa chama kina rasilimali nyingi zikiwemo maeneo ya uwekezaji kwa ajili ya majengo ya biashara na sekta ya utalii.

Alieleza kuwa huu ni wakati wa CCM kuingia rasmi katika mapinduzi ya kiuchumi kwa kuendana na maendeleo ya vyama vya ukombozi na vyama rafiki duniani, ikiwemo ANC na vyama vingine vyenye mafanikio makubwa kiuchumi.

Katika hatua nyingine, Dk. Mwinyi alisema Serikali inatarajia kujenga barabara ya kisasa ya njia nne kutoka Tunguu hadi Makunduchi kwa lengo la kuimarisha uchumi na kuongeza fursa za ajira na biashara kwa wananchi wa Mkoa wa Kusini Unguja.

Pia alisema Serikali ina mpango wa kumaliza changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama katika Mkoa huo kupitia upanuzi wa mtandao mkubwa wa usambazaji wa maji.

Alisema katika awamu yake ya pili ya uongozi ataendelea kutekeleza ahadi zote za maendeleo zilizomo katika Ilani ya CCM ya mwaka 2025/2030.

“Maendeleo sio vitu pekee, bali pia ni watu. Ndiyo maana Serikali imeongeza mshahara wa kima cha chini kutoka shilingi 300,000 hadi 500,000 ili kuboresha maisha ya wananchi,” alisema.

Aidha, alisema Serikali inatarajia kuongeza posho za wazee kulingana na ukuaji wa uchumi wa nchi.

Dk. Mwinyi alisisitiza kuwa ahadi zote zilizotolewa katika kampeni zilizopita zitafanyiwa kazi kwa vitendo ili kuiwezesha CCM kuingia katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2030 ikiwa na nguvu zaidi na kushinda kwa kishindo.

Pia alizitaka Kamati za Maadili za CCM katika ngazi zote kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa taratibu na kanuni za chama, badala ya kusubiri kuchukua hatua dhidi ya wanachama wakati wa uchaguzi pekee.

Akitoa salamu za CCM, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk. Mohamed Said Dimwa, alisema utekelezaji mzuri wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM umeendelea kuwa msingi muhimu wa maendeleo ya nchi.

Dk. Dimwa alisema Rais Dk. Mwinyi ameendelea kuwa mfano wa kiongozi mwenye maono, mchapa kazi na muadilifu, huku utendaji wake ukiendelea kuleta maendeleo endelevu kwa wananchi.

Kwa upande wake, Kaimu Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja, Abdallah Mwinyi Hassan, alisema wanachama wa CCM katika Mkoa huo wanajivunia mafanikio makubwa ya maendeleo yaliyotekelezwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Alisema kazi kubwa iliyopo sasa ni kuendelea kujipanga kimkakati ili CCM iendelee kuimarika kiitikadi, kiuchumi na kisiasa sambamba na kudumisha umoja na mshikamano ndani ya chama.