Na Mwandishi Maalumu – Njombe

9/5/2026 Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imewahimiza wananchi kujenga utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara kupitia kampeni ya “Jua Namba Zako” ili kubaini mapema vihatarishi vya magonjwa ya moyo na kupata matibabu kwa wakati.

Rai hiyo imetolewa leo na Daktari wa Taasisi hiyo Samweli Mbilinyi wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu huduma za upimaji wa moyo zinazotolewa na JKCI kwenye Kikao Kazi cha 21 cha Maafisa Habari, Mawasiliano, Itifaki na Uhusiano Serikalini kinachofanyika katika Hoteli ya Agreement iliyopo mjini Njombe.

Dkt. Mbilinyi alisema wananchi wengi bado hawana uelewa wa kutosha kuhusu magonjwa ya moyo jambo linalosababisha baadhi yao kuishi na matatizo hayo bila kujitambua hadi wanapofika hospitalini wakiwa na matatizo mengine.

Alitoa mfano wa mgonjwa aliyefika katika upimaji huo ambao huduma za upimaji wa magonjwa mbalimbali zinatolewa kwajili ya matatizo ya miguu lakini baada ya kupimwa alibainika kuwa na shinikizo kubwa la damu lililozidi kiwango cha kawaida hali iliyowalazimu wataalamu wa JKCI kumfanyia vipimo vya moyo na kuanza matibabu mara moja.

“Tumegundua wananchi wengi hawajawahi kupima afya ya moyo wala kufahamu viwango vyao vya afya. Kupitia kampeni ya Jua Namba Zako tunawahamasisha wananchi wajitokeze kupima ili kujua hali zao mapema na kupata tiba stahiki”, alisema Dkt. Mbilinyi.

Dkt. Mbilinyi alisema katika upimaji unaoendelea wamebaini watu wengi wenye shinikizo la juu la damu na matatizo ya moyo ambao hawakuwahi kufanyiwa vipimo vya moyo wala kujua hali zao za afya.

Aliishukuru Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kuwezesha upatikanaji wa dawa bure kwa wananchi wanaobainika kuwa na matatizo mbalimbali ya afya ikiwemo magonjwa ya moyo katika upimaji huo.

“Ninawaomba wananchi wajitokeze kwa wingi kupima afya zao. Watakaobainika kuwa na changamoto watapatiwa ushauri wa kitaalamu, tiba, dawa bila malipo na rufaa ya kwenda kutibiwa JKCI”, alisisitiza.

Kwa upande wao wananchi waliopata huduma hizo walieleza kufurahishwa na ujio wa wataalamu wa JKCI mkoani Njombe huku wakisema umewasaidia kupata huduma karibu na maeneo yao na kupunguza gharama za kusafiri kwenda Dar es Salaam.

Mmoja wa wananchi hao Farida Fredrick kutoka kijiji cha Ihalula, alisema alifika kupata huduma baada ya kusikia madaktari wa JKCI wanatoa huduma Njombe.

“Mimi ni mgonjwa wa moyo na huwa nahudhuria kliniki ya JKCI Dar es Salaam. Niliposikia madaktari wako hapa Njombe nikaona nitumie nafasi hii kupata huduma karibu na nyumbani, huduma ni nzuri sana na wananchi wengi wajitokeze kupima”, alisema Farida.

Joseph Mwakalonge mkazi wa Njombe mjini alisema alikuwa akisumbuliwa na maumivu ya kichwa pamoja na uchovu wa mara kwa mara bila kufahamu chanzo chake lakini baada ya kufanyiwa uchunguzi alibainika kuwa na shinikizo la juu la damu na kupewa matibabu.

“Naishukuru sana JKCI kwa kuleta huduma hizi karibu yetu. Sikuwahi kujua kama nina tatizo la presha kubwa kiasi hiki lakini leo nimepata elimu, vipimo na dawa kitu ambacho kitanisaidia kuutunza moyo wangu mapema ili usipate madhara zaidi”,alisema Mwakalobe.

Naye Rehema Mlowe mkazi wa Makambako alisema alikuwa hajawahi kupima afya ya moyo tangu alipogundulika kuwa na changamoto ya presha miaka miwili iliyopita lakini ujio wa madaktari wa JKCI umempa nafasi ya kufanyiwa uchunguzi wa kina na kupata ushauri wa namna ya kuishi kwa kufuata mtindo bora wa maisha.

“Nimepata huduma nzuri na wataalamu wanatoa elimu kwa upendo mkubwa. Ninawaomba wananchi wenzangu watumie fursa hii kuja kupima afya zao mapema kabla hali haijawa mbaya”, alisema Rehema.

Katika upimaji huo JKCI inatoa huduma za uchunguzi wa awali wa magonjwa ya moyo, uchunguzi wa shinikizo la damu, kipimo cha kuangalia uwingi wa sukari kwenye damu, kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi, elimu ya lishe bora na mtindo sahihi wa maisha, elimu ya kujikinga na magonjwa ya moyo na ushauri wa kitaalamu kutoka kwa madaktari bingwa wa moyo.