Imeelezwa kuwa Mikutano ya Mabaraza ya Wafanyakazi ni majukwaa muhimu ya kuwashirikisha watumishi moja kwa moja katika mipango ya Serikali ili kupata mawazo mapya na umiliki wa pamoja wa mipango hiyo kwa lengo la kutekelezwa kwa ufanisi na bila manung’uniko.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC), Mhe. James Millya wakati anafungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki jijini Dodoma Mei 08, 2026.
Mhe. Millya alisema kitendo cha Baraza hilo kupitia makadirio ya bajeti ya Mwaka wa Fedha 2026/2027 kitawapa watumishi fursa ya kupitia maeneo muhimu ya vipaumbele vilivyowekwa na kuboresha mikakati ya utekelezaji wake kwa kuzingatia Sera, Mikakati na Mipango iliyopo.
Mhe. Millya alitaja mafanikio mbalimbali kupitia utekelezaji wa mpango wa utekelezaji wa Mwaka wa Fedha 2025/2026 ambao utakamilika Juni, 30 2026. Mafanikio hayo ni pamoja na teuzi za nafasi za kikanda na kimataifa ikiwa ni pamoja uteuzi wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Balozi Stephen Mbundi; kuimarika kwa taswira na heshima ya Tanzania katika nyanja ya kimataifa; kuimarika kwa ushirikiano wa uwili, kikanda na kimataifa; na kuongezeka kwa mchango wa Watanzania waishio nje ya nchi.
Mafanikio mengine ni kuanza kwa ujenzi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mlima Kilimanjaro; ujenzi na ukarabati wa ofisi na makazi ya Balozi nje ya nchi; na kulinda usalama wa Watanzania nje ya nchi na kuwarejesha salama kutoka kwenye maeneo yenye changamoto za usalama.
Naibu Waziri Mallya alisisitiza umuhimu wa Wizara kuzingatia vipaumbele vya Serikali kuelekea utekelezaji wa bajeti ya Mwaka wa Fedha 2026/2027 na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 ambayo utekelezaji wake utaanza mwaka wa fedha ujao.

