📍Bungeni Dodoma
Suala la Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi limepewa umuhimu na mtazamo wa kipekee wakati wa mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia 2026/2027 katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliohitimishwa leo, tarehe 8 Mei 2026.
Akizungumza kabla ya kuhitimishwa kwa mjadala wa bajeti ya Wizara hiyo, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mheshimiwa Wanu Hafidh Ameir hali hiyo imejidhihirisha kwa wabunge kutoa michango mingi na kuuliza maswali mengi zaidi kuhusiana na VETA, ambapo asilimia 62.96 ya maswali yaliyoulizwa yalihusiana na VETA.
“Kati ya maswali 27 yaliyoulizwa na waheshimiwa wabunge, 17 yalielekezwa VETA,” amesema.
Akifafanua kuhusu baadhi ya maeneo, Mheshimiwa Wanu Ameir amesema ujenzi wa awamu ya kwanza wa vyuo 65 vya VETA unatarajiwa kukamilika Septemba 2026 na kwamba fedha ya kumalizia ujenzi huo imeshapatikana.
Kuhusu rasilimali watu kwa ajili ya kuendesha mafunzo ya ufundi stadi, Mheshimiwa Wanu Ameir amesema mwaka huu Serikali imepata kibali cha kuajiri wakufunzi 770 wa vyuo vya ufundi stadi.
Vilevile, Mheshimiwa Wanu Ameir amebainisha kuwa Shilingi Bil 150.3 zimetengwa kupitia mradi wa ESPJ II kutumika katika nunuzi wa vifaa kwa ajili ya vyuo vya VETA.
Sambamba na hayo, amebainisha kuwa VETA imeingia makubaliano na viwanda takribani 87 kwa ajili ya kushirikiana katika utoaji mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi.

