WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amefanya ukaguzi wa daraja la Magole lililopo Dumila katika Mto Mkundi wilayani Kilosa na kuagiza uongozi wa TANROADS utafute suluhu ya kudumu ya changamoto inayolikabili daraja hilo ya kujaa maji na mchanga kila mwaka.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Ijumaa, Mei 8, 2026) wakati akizungumza na wananchi waliofika darajani hapo kumsikiliza na akamtaka Meneja wa TANROADS Mkoa wa Morogoro ashirikiane na wataalamu wengine kuandaa utaratibu wa kuwaruhusu wananchi kuchimba mchanga katika eneo hilo kwa kuzingatia maelekezo ya kitaalamu, ili kusaidia kupunguza mzigo wa gharama za Serikali na wakati huohuo kulinda miundombinu ya daraja hilo.
“Meneja wa TANROADS na wenzako wote ratibuni eneo ambalo tunahangaika kutoa mchanga na hatuna bajeti, wananchi muwaruhusu watoe mchanga huo kwa utaratibu wa kitaalamu,” amesisitiza Waziri Mkuu.

