Mbunge wa Viti Maalum, Cecilia Pareso(CCM) amesema mabadiliko ya sera ya elimu yaliyofanywa chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan yameleta maboresho makubwa katika sekta ya elimu nchini.
Akichangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Elimu bungeni, Pareso ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bunge, amesema hapo awali kulikuwa na malalamiko mengi kuhusu mfumo wa elimu na mitaala, lakini Serikali ya Rais Samia imefanya maboresho makubwa yaliyolenga kuendana na mahitaji ya sasa.
Amesema hatua ya kuruhusu wanafunzi waliopata ujauzito kurejea shuleni imefungua fursa kwa maelfu ya watoto wa kike kuendelea kutimiza ndoto zao za elimu baada ya awali kukatisha masomo kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ndoa za utotoni, ukatili na umasikini.
Pareso,amesema takwimu zinaonesha kuwa zaidi ya wanafunzi 4,000 walikuwa wanakatisha masomo kutokana na changamoto hizo, hali iliyochochea maboresho ya sera ya elimu ili kuhakikisha hakuna mtoto anayekosa haki ya elimu.
Amesema hadi sasa zaidi ya wanafunzi 10,000 wamerejeshwa shuleni, jambo ambalo linaonesha dhamira ya Rais Samia kuhakikisha watoto wote wanapata elimu bila ubaguzi.
Aidha, amepongeza juhudi za Serikali katika kuimarisha elimu ya ufundi na stadi za kazi kupitia ujenzi wa vyuo vya VETA nchini kote, akisema hatua hiyo inaonesha Serikali inatambua umuhimu wa ujuzi katika kukuza ajira na maendeleo ya vijana.
Pareso amesema maboresho hayo ya sera ya elimu ni sehemu ya mafanikio makubwa ya Serikali ya Rais Samia katika kuhakikisha mfumo wa elimu unakuwa jumuishi na wenye kutoa fursa sawa kwa wote.