DSM 8 Mei, 2026
Waziri wa Afya, Mheshimiwa. Mohamed Omary Mchengerwa, amezindua Mfuko wa Bima ya Afya wa Mufti
na amepongeza juhudi za Jumuiya ya Kiislamu nchini kwa kuanzisha, akieleza kuwa hatua hiyo ni mchango
mkubwa katika juhudi za Taifa katika kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma bora za afya bila
vikwazo vya kifedha.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Mfuko huo tarehe 7 Mei 2026 jijini Dar es Salaam, Mheshimiwa
Mchengerwa alisema kuwa ushiriki wa taasisi za dini katika sekta ya afya unaonesha namna jamii inavyoweza kushirikiana na Serikali katika kulinda afya na ustawi wa wananchi. Afya ni Msingi wa Maendeleo ya Taifa
Katika hotuba yake, Waziri Mchengerwa alisisitiza kuwa afya bora ndiyo msingi wa maendeleo ya mtu mmoja mmoja, familia na Taifa kwa ujumla. Alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Samia
Suluhu Hassan imeendelea kuweka mkazo mkubwa katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya zenye ubora bila kubebeshwa gharama kubwa wanapougua.
Kwa mujibu wa Mheshimiwa Mchengerwa, uwekezaji katika afya si suala la tiba pekee bali ni uwekezaji katika nguvu kazi, ustawi wa jamii na maendeleo endelevu ya nchi. Taasisi za Dini Zatajwa kuwa Nguzo ya Ustawi wa Jamii
Aidha, Mheshimiwa Mchengerwa aliipongeza Jumuiya ya Kiislamu kwa kuonesha mfano wa uongozi wenye maono kupitia kuanzishwa kwa Mfuko huo, akibainisha kuwa tayari baadhi ya wananchi wameanza kunufaika na huduma zinazotolewa.
Alisema taasisi za dini zimeendelea kuwa nguzo muhimu katika kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kutunza afya, kufanya uchunguzi wa afya mapema na kuhamasisha wananchi kujiunga na mifumo ya bima ya afya.
Akizungumza kuhusu nafasi ya dini katika ustawi wa jamii, Waziri huyo alieleza kuwa mafundisho ya dini
zote yanahimiza kulinda afya na kuthamini uhai wa mwanadamu. Alikumbusha kuwa katika mafundisho ya Kiislamu, afya hutajwa kuwa miongoni mwa neema kubwa ambazo watu wengi huzipuuzia, huku mafundisho ya Kikristo nayo yakisisitiza wajibu wa kulinda afya kama sehemu ya kuthamini maisha aliyotoa Mungu.
Wito wa Uwajibikaji na Usimamizi Bora Katika hatua nyingine, Waziri Mchengerwa alisisitiza umuhimu wa uwazi, uwajibikaji na usimamizi madhubuti wa Mfuko huo ili kuhakikisha wananchi wanaoweka imani yao katika mfumo wa bima wanapata huduma stahiki kwa haki na usawa.
Alieleza kuwa mafanikio ya Mfuko huo hayatapimwa kwa ukubwa wa hafla ya uzinduzi, bali kwa idadi ya wananchi watakaopata msaada wa matibabu, familia zitakazolindwa dhidi ya gharama kubwa za afya na maisha yatakayookolewa kupitia huduma za bima.
“Wananchi wanahitaji kuona matumizi sahihi ya rasilimali na huduma zinazorejesha matumaini kwa wale waliokuwa wakikosa uwezo wa kumudu gharama za matibabu,” alisisitiza. Mfuko wa Mufti Waungwa Mkono Katika Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote
Waziri huyo alisema uzinduzi wa Mfuko huo umefanyika wakati Serikali ikiwa inaendelea kutekeleza Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, Sura ya 161, ambayo inalenga kuhakikisha kila Mtanzania anakuwa na kinga ya bima ya afya.
Alieleza kuwa utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mpango huo ulianza Januari 2026 kwa kuwahusisha wananchi wasio na uwezo wa kugharamia huduma za bima ya afya. Aidha, sheria hiyo imefungua fursa kwa skimu za bima za umma na binafsi, ikiwemo zinazomilikiwa na taasisi za dini, kusajiliwa rasmi na kushiriki katika utekelezaji wa mpango wa Taifa wa Bima ya Afya kwa Wote.
Mchengerwa alitoa rai kwa viongozi wa Mfuko wa Bima ya Afya wa Mufti kuhakikisha skimu hiyo inasajiliwa na Tanzania Insurance Regulatory Authority ili iwe sehemu rasmi ya utekelezaji wa mfumo wa bima ya afya nchini. Elimu ya Bima ya Afya Yatajwa kuwa Muhimu
Aidha, Mchengerwa aliwahimiza viongozi wa dini na wananchi kwa ujumla kuendelea kuelimishana kuhusu umuhimu wa bima ya afya na kuelewa kwa kina mafao yanayotolewa na mifuko mbalimbali ya bima.
Alisisitiza kuwa elimu hiyo itasaidia wananchi kufanya maamuzi sahihi kuhusu vifurushi vya huduma wanavyovichagua na kupunguza changamoto za kukosa huduma muhimu wakati wa mahitaji.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, kueneza elimu ya bima ya afya ni sehemu ya kujenga jamii yenye ustawi, mshikamano na usalama wa kijamii.
Serikali Yaahidi Kuendeleza Ushirikiano Akihitimisha hotuba yake, Mchengerwa alisema Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na taasisi za dini pamoja na wadau wengine katika kufanikisha lengo la kuhakikisha kila mwananchi anapata bima ya afya.
Aliutakia mafanikio Mfuko wa Bima ya Afya wa Mufti na kueleza matumaini kuwa mfuko huo utakuwa chachu ya kuimarisha afya bora, matumaini na ustawi wa wananchi wengi zaidi nchini Tanzania.
