Katika kuongeza juhudi za kuitangaza Tanzania kimataifa ili kufikia lengo la watalii milioni 8 mwaka 2030, leo jioni hii Mei 7, 2026, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, katikati ya Mkutano wa Baraza la Utalii na Usafiri Duniani (WTCC), amekutana na kampuni kubwa za kutangaza utalii duniani.
Taasisi ya kwanza ni ya Peter Greenberg Worldwide iliyoko California, Marekani, ambapo katika mazungumzo na Mwanzilishi wa kampuni hiyo Bw. Peter Greenberg, viongozi hao wamejadili kuanzia mafanikio ya filamu ya “Tanzania: The Royal Tour,” hadi namna bora ya kuendeleza hatua zijazo za filamu hiyo iliyokonga nyoyo za wengi ndani na nje ya nchi.
Aidha, amekutana pia na Bw. Nick Evans, Mwanzilishi wa taasisi ya Beautiful Destinations, yenye ofisi katika miji ya New York, London na Dubai, ikiwa imejikita katika matangazo ya utalii kwa njia za ubunifu, matumizi ya akili-unde na ikijivunia mtandao wa watozi zaidi ya 500 wa maudhui ya kiutalii kutoka maeneo mbalimbali duniani.
Mkutano huo wa kimkakati wa WTTC unaowakutanisha wadau wa utalii na viongozi wa Serikali umeendelea leo kwenye meli inayotembea ya Crystal Serenity ambayo imefika katika Mji wa Bandari wa Port Said ambapo jana ilianzia katika Bandari ya Sukhna na kesho utahitimishwa katika mji wa Bandari wa Alexandria yote ikiwa nchini Misri.

