Na Maelezo Zanzibar 06.05.2026 

Matumizi ya nishati safi ya kupikia imeendelea kuleta mafanikio katika jamii ambapo wananchi wa kijiji cha Bumbwini Kiyongwe wanamefaika kiafya, kiuchumi na kimazingira kupitia matumizi ya majiko yanayotumia makaa mbadala salama kwa kupikia.

Kauli hiyo imetolewa na Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Maandalizi na Msingi Kiyongwe Bumbwini, Abass Rajab Pande Wilaya ya Kaskazini B Unguja, wakati wa ziara ya kutembelea skuli zilizopatiwa majiko hayo kupitia mradi wa nishati safi.

Amesema matumizi ya nishati hiyo yamesaidia kuboresha afya za watumiaji kwa kupunguza madhara yatokanayo na moshi wa kuni na makaa ya kawaida pamoja na kupunguza gharama za maandalizi ya chakula na kuokoa muda wakati wa kupika.

Aidha Mwalimu Pande amesema kuwa hatua hiyo imechangia kuwasaidia wanafunzi kuhudhuria masomo yao kwa wakati kutokana na urahisi wa kuandaa chakula kwa muda mfupi.

Ameeleza kuwa skuli hiyo huandaa uji na viazi lishe kwa wanafunzi wa maandalizi na msingi ambapo jumla ya wanafunzi 676 hutumia huduma hiyo na kupata chakula kila siku.

“Matumizi ya majiko haya hayabadilishi ladha ya chakula. Chakula hubaki na ladha ile ile kama kinavyopikwa kwa kutumia kuni,” amesema Mwalimu Pande.

Aidha, ameitaka jamii kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia kwa kutumia nishati safi kama makaa mbadala, gesi na umeme ili kupunguza ukataji miti holela unaochangia uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi.

“Nimehamasika kutumia kuni hizi mbadala hivyo tunahitaji kutengenezewa majiko madogo kwa matumizi ya majumbani ili kurahisisha shughuli za mapishi,” ameongeza.

Naye Mpishi wa uji na Mwalimu wa Lishe katika Skuli ya Maandalizi Kiyongwe Mtumwa Khamis Kai, amesema majiko hayo yameleta nafuu kubwa kwa wapishi kwa kuondoa usumbufu wa moshi na joto kali lililokuwa likiwakabili hapo awali.

“Tumeondokana na moshi mkubwa uliokuwa ukitusababishia matatizo ya kifua na makamasi hivi sasa tunapika kwa haraka na kazi inamalizika kwa muda mfupi” ameeleza Bi. Mtumwa.

Kwa upande wake, mwanafunzi wa skuli hiyo Zidadu Abdalla Pande, amesema matumizi ya nishati hiyo imewasaidia wanafunzi kutotumia muda mwingi kutafuta kuni na kuwahi mapema masomo darasani.

Mradi huo umefadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Mitaji ya Maendeleo (UNCDF) ambapo skuli nne za Mkoa wa Kaskazini Unguja zimepatiwa majiko hayo, zikiwemo Skuli ya Kiyongwe, Donge, Kigunda na Nungwi.