Na. Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Bungeni Dodoma
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof . Adolf Mkenda amesema kuwa Serikali itaendelea kuimarisha sekta ya elimu katika ngazi zote kuanzia elimu ya awali, msingi, sekondari hadi elimu ya juu kupitia uwekezaji mkubwa wa miundombinu, mafunzo na ubora wa ufundishaji.
Amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2026/27, Serikali imepanga kujenga madarasa 1,360 ili kusaidia utekelezaji wa sera ya elimu ya miaka 10 ya lazima, pamoja na kujenga mabweni 17 katika shule za sekondari na nyumba 33 za walimu ili kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.
Akiwasilisha Bajeti ya Wizara hiyo Mei 7,2026 bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda,Aidha amebainisha kuwa pia ameongeza kuwa vituo 50 vya walimu vitajengwa katika halmashauri mbalimbali ili kuimarisha usimamizi wa elimu.
Ameeleza kuwa Serikali itaendelea kuboresha ubora wa elimu kwa kufanya tathmini katika taasisi zaidi ya 7,000 za elimu nchini pamoja na kuimarisha ofisi za uthibiti ubora wa shule katika baadhi ya maeneo ya kimkakati. Pia amesema kuwa mkazo utawekwa katika kuimarisha stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa kuwajengea uwezo walimu zaidi ya 1,300 kutumia mbinu bunifu za ufundishaji.
Aidha amebainisha kuwa Serikali itaongeza upatikanaji wa vitabu vya kiada zaidi ya milioni 8 ili kufikia uwiano wa mwanafunzi mmoja kitabu kimoja, sambamba na kuanzisha vitabu vya kidigitali vyenye maudhui shirikishi kama video, sauti na majaribio ya kielektroniki ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia katika elimu.
Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha taaluma ya ualimu kupitia mafunzo ya vitendo kwa walimu tarajali, pamoja na kutoa ufadhili wa masomo kwa walimu zaidi ya 1,200 na mafunzo ya stadi mbalimbali kwa maelfu ya watumishi wa elimu. Pia amesema elimu ya watu wazima na elimu mbadala itaongezewa fursa ili kuwafikia vijana waliokosa nafasi katika mfumo rasmi.
Katika elimu ya juu, Waziri Mkenda amesema Serikali itaongeza udahili wa wanafunzi 180,000 na kuongeza mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu hadi zaidi ya 290,000, huku ikipanua ufadhili katika fani za Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM) ili kuandaa wataalamu watakaosaidia maendeleo ya taifa.
