Na. Meleka Kulwa- Fullshangwe Blog, Dodoma
Serikali imesema ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha mfumo wa sheria na sera maalum zitakazosimamia huduma za upandikizaji wa viungo nchini, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha huduma za kibingwa katika sekta ya afya.
Akizungumza katika ufunguzi wa kongamano la kimataifa la kisayansi lililoandaliwa na Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa, Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe amesema kuwa maandalizi ya mfumo huo yanatarajiwa kukamilika ifikapo Septemba mwaka huu.
Amesema kuwa uwepo wa sheria na sera hizo utaweka msingi imara wa utoaji wa huduma za upandikizaji viungo kwa kuzingatia viwango vya kitaifa na kimataifa, hali itakayosaidia kuongeza ubora na usalama wa matibabu kwa wagonjwa.
Aidha, amebainisha kuwa Tanzania imeendelea kupiga hatua katika utoaji wa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi, jambo ambalo limepunguza utegemezi wa wagonjwa kwenda nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.
Ameongeza kuwa tayari huduma za upandikizaji wa uloto kwa wagonjwa wa saratani ya damu pamoja na upandikizaji wa figo zinaendelea kutolewa nchini, huku mipango ya kuanzisha huduma za upandikizaji wa ini na moyo ikiendelea.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa, Prof. Abel Makubi amesema kuwa uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali katika sekta ya afya umechangia kuboresha huduma za kibingwa nchini.
Baadhi ya wagonjwa waliopata huduma hizo wameeleza namna matibabu hayo yalivyobadilisha maisha yao.
Miongoni mwao ni Richard Masimba ambaye amesema baada ya kufanyiwa upandikizaji wa figo miezi sita iliyopita ameweza kurejea katika maisha yake ya kawaida.
