Na Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Dodoma
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kuwa kinaunga mkono ripoti ya Tume ya Uchunguzi wa matukio ya ghasia yaliyotokea Oktoba 29, 2025, huku kikisisitiza umuhimu wa maridhiano ya kitaifa pamoja na kuendelea kwa uchunguzi wa kina ili kubaini ukweli wa matukio hayo.
Akizungumza na waandishi wa habari Mei 4, 2026 jijini Dodoma, Katibu wa NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi, amesema kuwa chama hicho kimeipokea ripoti hiyo kwa uzito mkubwa kutokana na umuhimu wake katika kuimarisha mshikamano, amani na umoja wa kitaifa.
Amesema kuwa lengo la tume hiyo lilikuwa ni kusaidia taifa kujifunza kutokana na matukio yaliyotokea na kuweka msingi bora wa kuendeleza mshikamano kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Aidha, amebainisha kuwa CCM inampongeza Mwenyekiti wa chama hicho na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuunda tume hiyo kwa kuzingatia sheria za nchi, hatua ambayo imeonesha dhamira ya dhati ya kuhakikisha haki, uwazi na uwajibikaji vinazingatiwa.
Pia ameongeza kuwa chama hicho kimeridhishwa na namna tume hiyo ilivyotekeleza majukumu yake kwa uhuru, weledi na uzalendo mkubwa chini ya Mwenyekiti wake, Jaji Mkuu mstaafu Mohamed Othman Chande pamoja na wajumbe wote wa tume hiyo.
KihongosiKihongosi amesema kuwa CCM inawapongeza Watanzania waliojitokeza kutoa ushahidi na maoni yao kwa utulivu na ushirikiano mkubwa, hali iliyosaidia kukamilika kwa kazi ya tume hiyo kwa mafanikio.
Amesema kuwa chama hicho kinaunga mkono mapendekezo yote yaliyotolewa na tume hiyo na kumshukuru Rais Samia kwa kuyaokea na kuonesha utayari wa kuyafanyia kazi kwa manufaa ya taifa.
Aidha, amebainisha kuwa CCM ipo tayari kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa mapendekezo hayo pamoja na kuhamasisha wananchi kuendelea kudumisha amani, upendo na mshikamano wa kitaifa.
Aidha, Ameeleza kuwa pamoja na hatua zilizofikiwa, bado kuna umuhimu wa kuendelea na maridhiano ya kitaifa sambamba na uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo halisi cha ghasia hizo, wahusika wake pamoja na malengo yaliyokuwa nyuma ya matukio hayo.
Pia ameongeza kuwa CCM inaunga mkono kuundwa kwa tume ya upelelezi itakayofanya uchunguzi wa kina zaidi kuhusu matukio hayo, huku ikieleza utayari wake wa kushirikiana na wadau mbalimbali kwa ajili ya kulinda amani na mshikamano wa taifa.
