Na. Meleka Kulwa- Fullshangwe Blog, Dodoma 

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Makonda, Amezindua ofisi mpya za Jumuiya ya Wanahabari ya Mitandao ya kijamii Tanzania (JUMIKITA),Tawi la Dodoma aidha ameitaka JUMIKITA kutumia mitandao ya kijamii kujenga jamii yenye maadili na kuendelea kulinda utamaduni wa Kitanzania kupitia matumizi sahihi ya Kiswahili.

Ameyasema hayo Mei 3, 2026 jijini Dodoma wakati akizindua ofisi za JUMIKITA Tawi la Dodoma katika eneo la Ilazo.Aidha, amebainisha kuwa Kiswahili ni sehemu ya utambulisho wa taifa na Afrika kwa ujumla, huku akibainisha kuwa Tanzania kupitia UNESCO imeendelea kupewa heshima kubwa katika kukuza lugha hiyo duniani.

Ameongeza kuwa mwaka huu Tanzania inatarajia kushiriki maadhimisho ya Kiswahili duniani yatakayofanyika mjini Paris, Ufaransa, Aidha, Makonda amebainisha kuwa mitandao ya kijamii inapaswa kutumika kuelimisha na kujenga jamii badala ya kusambaza maudhui yanayoharibu maadili ya taifa.

Amesema kuwa wanamitandao wanapaswa kuwa mabalozi wa maadili kwa kuhakikisha maudhui wanayochapisha yanazingatia mila, desturi na misingi ya jamii ya Kitanzania.

“Tunataka mitandao itumike kujenga taifa letu, kuonesha fursa zilizopo nchini na kuhamasisha maendeleo ya jamii,” amesema Makonda.

Pia amesisitiza umuhimu wa wanahabari na watengeneza maudhui kufanya kazi kwa weledi na kuacha tabia ya kutumia taarifa zinazochochea migogoro kwa ajili ya maslahi binafsi.

Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuwawezesha vijana wa mitandao kwa kuwapatia mikopo na fursa mbalimbali zitakazowasaidia kukuza kazi zao na kuchangia maendeleo ya taifa.

Waziri Makonda amesema kuwa  Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kufungua milango kwa vijana wa mitandao ili waweze kutumia vipaji vyao kujenga uchumi na kuitangaza Tanzania kimataifa.

Aidha, ametoa wito kwa JUMIKITA kuendelea kushirikiana na Serikali katika kulinda maadili, kuhamasisha uzalendo na kutumia mitandao ya kijamii kwa manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla.