Na.Sophia Kingimali 

Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam, John Rioba Mrema, amewataka vijana wanaosoma katika Chuo cha VETA Furahika kutumia fursa ya elimu waliyonayo kujenga maisha yao na kuepuka kukata tamaa kutokana na changamoto wanazokutana nazo.

Akizungumza kwa niaba ya Meya , Juma Ali maarufu kama Shetta,kwenye mahafali ya chuo cha veta Furahika Jijini Dar es salaam Mrema amesema wanafunzi wanapaswa kuwa na ndoto kubwa na kuamini katika uwezo wao, akisisitiza kuwa dunia ya sasa imejaa fursa nyingi zinazohitaji ubunifu na uthubutu wa vijana.

 “Niwatie moyo wanafunzi mnaosoma hapa najua wengi ni wale ambao hamna uwezo lakini niwaambie inawezekana kabisa kutoka sifuri hadi kufikia mafanikio makubwa kama utakuwa na nidhamu na bidii,” alisema.

Aidha, amewahimiza wanafunzi kuendelea kutafuta maarifa hata nje ya darasa kwa kutumia teknolojia na vyanzo mbalimbali vya kujifunzia huku akisisitiza kuwa elimu ndiyo silaha pekee ya kupambana na umaskini.

Katika hotuba yake, Mrema pia aligusia umuhimu wa wazazi katika malezi na mafanikio ya watoto wao, akibainisha kuwa mchango wa wazazi, hususan mama, una nafasi kubwa katika kufanikisha ndoto za vijana.

Sambamba na hayo Mrema alieleza kuvutiwa na ubora wa wahitimu wa chuo hicho baada ya kukutana na mmoja wa wahudumu wa hoteli jijini Dar es Salaam aliyemvutia kwa huduma nzuri na baadaye kubaini kuwa alisoma katika chuo hicho, jambo lililomhamasisha kufika na kujionea mazingira ya ufundishaji.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha VETA Furahika, David Msuya, aliwataka viongozi na wadau mbalimbali kuendelea kupeleka vijana katika chuo hicho ili wapate ujuzi utakaowasaidia kujiajiri na kupunguza tatizo la ajira mitaani.

Msuya alisisitiza kuwa maendeleo hayana chama, hivyo ni muhimu kwa viongozi wa vyama vyote kushirikiana katika kuwawezesha vijana kupata elimu ya ufundi stadi kwa manufaa ya taifa.