Na Mwandishi Wetu,Mbinga
WANAFUNZI wa fani ya utabibu,uuguzi na ukunga wanaosoma katika chuo cha afya Litembo wilayani Mbinga,wameiomba Serikali kuhakikisha inatoa mikopo kwa wanafunzi wa fani hizo na kutoa ruzuku sawa kwa vyuo vya afya hapa nchini ili viweze kudahili wanafunzi wengi wa fani hiyo.
Ombi hilo limetolewa jana na makamu wa Rais wa Serikali ya wanafunzi wa chuo cha Afya Litembo kilichopo kijiji cha Litembo Halmashauri ya wilaya Mbinga mkoani Ruvuma Joseph Milinga,alipokuwa akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wengine waliokosa mkopo wa Serikali.
Alisema,kwenye fani ya maabara wamepata mikopo inayowasaidia kutatua changamoto ya ada,hata hivyo baadhi yao na wale wanaosoma fani ya uuguzi na utabibu hawajapata kabisa mikopo hiyo.
Alisema,ingawa Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeonyesha kuwajali,lakini kuna jambo la kufanya ili kuwawekea mazingira mazuri wanafunzi wa fani ya uuguzi,ukunga na utabibu ambao hawapati mikopo na hawanufaika na uwekezaji wa Serikali kwenye sekta ya elimu.
Alisema,iwapo Serikali itawekeza zaidi kwenye fani hizo na kuwapa mikopo wanafunzi wengi wa fani ya utabibu na uuguzi na ukunga wapatatikana wataalamu wengi ambao watakwenda kuwahudumia watanzania wenzao kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini.
“Hali ya mikopo kwa wanafunzi wa fani hizo hairidhishi kabisa na takwimu zinaonyesha katika chuo chetu wanafunzi wengi wanatoka kwenye familia maskini ambazo zinazotegemea kilimo,hivyo tunaiomba Serikali itoe mikopo kwa wanafunzi wote bila kubagua ili tuweze kutimiza malengo yetu”alisema.
Mwanafunzi mwingine Witness Ngalomba alisema,kozi zao ni za muda mrefu,hivyo mwanafunzi kama hana mazingira mazuri kifedha lazima atashindwa kuendelea na masomo,atarudi nyumbani na atakatisha ndoto za maisha yake na familia kwa ujumla.
Alisema,fani ya ukunga,uuguzi na utabibu zinahitaji vifaa maalum vya kuwawezesha kusoma kwa vitendo,hivyo Serikali inapaswa kuwasaidia kupata vifaa vinavyohitajika kwenye masomo kwa kutoa mikopo kwa wanafunzi wa fani hizo.
Ngalomba,amelishukuru Kanisa Katoliki Jimbo la Mbinga kuwajengea chuo hicho kwani wanafunzi wengi wanaomaliza kidato cha sita katika Mkoa wa Ruvuma na mikoa mingine ya jirani wanapata fursa ya kujiunga na chuo hicho kwa ajili ya kupata elimu ya juu.
Mkuu wa chuo Sista Lamberta Mlelwa alisema,sio wanafunzi wote wanaojiunga na chuo hicho wanatoka familia zenye uwezo kuna wakati mwanafunzi anafika mwaka wa pili au wa tatu anapata changamoto ya kuendelea na masomo kutokana na kushindwa kulipa ada hivyo analazimika kuahirisha masomo.
“Wanafunzi wengi tunaowapata wanatoka ukanda huu wa Mbinga ambao ni watoto wa wakulima,hawana uwezo mkubwa kifedha na wazazi wao wanategemea zaidi kilimo,kwa hiyo wanapofika shuleni wanakumbuna na changamoto ya ada ambayo inapelekea kutokuja chuoni kwa wakati”alisema.
Alisema,hata wanapofanya mawasiliano na wazazi wao majibu wanayopata ni hali duni ya maisha ambayo inasababisha kukosa fedha za kulipa ada ya watoto wao.
“Naiomba Serikali, kwa kuwa imeweka utaratibu wa kutoa mkopo kwa kozi za maabara,ni vizuri itoe mikopo kwa fani ya utabibu,ukunga na uuguzi kwani zina muhimu kwenye jamii yetu,mikopo itawasaidia watoto wengi wa wakulima ambao wanatamani sana kusoma fani hizo”alisema.

