NA DENIS MLOWE ,IRINGA 
MKUU wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amethibitisha ujio wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwigulu Lameck Nchemba, ambaye anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi mkoani humo kuanzia Mei 2 hadi Mei 3.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mkuu wa Mkoa amesema ziara hiyo ni tukio muhimu litakalogusa maeneo mbalimbali ya mkoa, hususan katika Wilaya zote za mkoa wa Iringa. 
Alisema kuwa katika ziara hiyo ataanza na wilaya ya Mufindi ambapo Waziri Mkuu anatarajiwa kutembelea halmashauri zote mbili za wilaya hiyo, ambazo ni Halmashauri ya Mji Mafinga na Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, pamoja na kufanya mikutano ya hadhara katika majimbo matatu ,Jimbo la Mafinga Mjini, Jimbo la Mufindi Kusini na Jimbo la Mufindi Kaskazini.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, siku ya Mei 2 Waziri Mkuu atawasili rasmi mkoani Iringa na atafanya mkutano wa hadhara wa kusikiliza kero na maoni ya wananchi katika Kijiji cha Igowole, kilichopo Jimbo la Mufindi Kusini. Wananchi wa eneo hilo na maeneo ya jirani wametakiwa kujitokeza kwa wingi ili kushiriki mkutano huo muhimu wa viongozi na wananchi.
Katika siku hiyo hiyo, Waziri Mkuu anatarajiwa kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Mtili hadi Ifwagi na baadaye kuzungumza na wananchi wa Jimbo la Mufindi Kaskazini, ambako pia atapokea taarifa mbalimbali za miradi ya maendeleo na changamoto zinazoikabili jamii.
Siku ya Mei 3, Waziri Mkuu atafanya mkutano mwingine wa hadhara katika Jimbo la Mafinga Mjini, ambapo ataongea na wananchi na kupokea taarifa za sekta mbalimbali za serikali. 
Kheri James amewahamasisha wananchi wote wa Mkoa wa Iringa kujitokeza kwenye mikutano hiyo ili kupata fursa ya kusikiliza maelekezo ya serikali, kutoa hoja na kupata ufafanuzi wa kisera kutoka kwa Waziri Mkuu.
Aidha, wakuu wote wa taasisi, idara na sekta za serikali wametakiwa kuhudhuria mikutano yote ili kutoa majibu na ufafanuzi wa hoja zitakazowasilishwa na wananchi.
Mkuu wa Mkoa ameongeza kuwa Iringa imejiandaa kikamilifu kupokea ugeni huo wa kitaifa, akiutaja kuwa ni ugeni wenye manufaa makubwa kwa wananchi na kwa mustakabali wa maendeleo ya mkoa.
Amesema mkoa unamkaribisha Waziri Mkuu kwa mikono miwili na unatarajia ushiriki mkubwa wa wananchi katika shughuli zote za ziara hiyo.