‎‎Na. John Bukuku- Dar es salaam
‎
‎Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amewaomba Watanzania kuendelea kuimarisha umoja na mshikamano na wasitoe nafasi ya kuvurugwa na maadui wa nchi, akisema kuwa yaliyotokea Oktoba 29 yalitikisa Taifa na yameacha funzo.
‎
‎Ameyabainisha hayo Aprili 23, 2026 Ikulu jijini Dar es Salaam baada ya kupokea ripoti ya Tume ya kuchunguza matukio ya Oktoba 29, 2025, ambapo amesema kuwa “Ndugu zangu Watanzania umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu, niwaombe sana tuendelee kuimarisha umoja na mshikamano wetu, tusitoe nafasi ya kuvurugwa na maadui wa nchi yetu.”
‎
‎
‎Ameongeza kuwa “Tutakuwa tunajidanganya tusiposema ukweli kuwa yaliyotokea Oktoba 29 yalitikisa Taifa letu, yalitutikisa. Kupotea njia ndio kujua njia, tumegusa kaa la moto na tumejifunza,”
‎Aidha amebainisha kuwa Tume hiyo imesema uchunguzi umebaini ghasia zilipangwa, ziliratibiwa, zilifadhiliwa na kutekelezwa na watu wenye mafunzo na malengo yalikuwa kuvuruga uchaguzi.
‎
‎Rais Samia pia amesema kuwa ingewezekana siku kurudi nyuma, asingetamani matukio ya Oktoba 29, 2025 yatokee, akisema historia ingepaswa kuandikwa upya ili kufuta doa lililotokea kutokana na ghasia wakati na baada ya uchaguzi mkuu.
‎
‎Ameongeza kuwa walioumia ni Watanzania wenyewe, akisema waliopoteza watoto, ndugu, jamaa na marafiki ni Watanzania wote, na kwamba haiwezekani mtu mwingine asiye Mtanzania kuwa na uchungu zaidi kuliko wenyewe.
‎
‎Aidha amebainisha kuwa Watanzania walionesha uvumilivu na imani kwa Serikali licha ya hamasa zilizokuwa zikitolewa mitandaoni wakati wakisubiri ripoti hiyo.
‎
‎Rais Samia pia amerejea falsafa ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akibainisha kuwa umoja na mshikamano hufanya Taifa kuwa imara na kuwa vigumu kunyonywa kisiasa au kiuchumi, akisema migogoro katika baadhi ya mataifa imechangia umaskini.
‎
‎Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kushughulikia changamoto za kijamii kwa kuunda Tume ya Maridhiano itakayofanya uchunguzi wa kina kuhusu matukio mbalimbali ili kuwezesha mjadala wa kitaifa wa kurejesha amani.
‎Amebainisha kuwa Tume hiyo itazingatia pia ripoti ya Oktoba 29 iliyobaini viashiria vya tuhuma za jinai, pamoja na kushughulikia watu waliopotea au wanaodaiwa kutekwa, miili isiyopatikana na waliopoteza maisha kutokana na ghasia.
‎
‎Aidha amesema kuwa Tume hiyo itahusisha mpango wa kusaidia majeruhi wakiwemo waliopata ulemavu wa kudumu pamoja na wafanyabiashara walioathirika kurejea katika maisha yao ya kawaida, pamoja na askari waliopata madhara.