Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo, akizindua rasmi kampeni ya “Linda Ushirika, Chagua Uadilifu” Aprili 24,2026, jijini Dodoma katika Mkutano wa Wadau wa Maendeleo ya Ushirika.
Na. Meleka Kulwa- Fullshangwe Blog, Dodoma
Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) imezindua rasmi kampeni ya “Linda Ushirika, Chagua Uadilifu” uzinduzi huo umefanywa na Waziri wa Kilimo Mhe. Daniel Chongolo.
Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo, amesema kuwa kuna umuhimu wa kuimarisha ulinzi na usimamizi wa vyama vya ushirika kupitia kuanzishwa kwa ofisi maalum za taasisi mbalimbali zinazohusika na usimamizi na udhibiti.
Ameyabainisha hayo Aprili 24 jijini Dodoma, katika Mkutano wa Wadau wa Maendeleo ya Ushirika,
Amesema kuwa, “tunaweza kuwa na ofisi maalum za Takukuru kwenye maeneo ya ushirika ili kulinda thamani na mali za wanachama,” aidha amebainisha kuwa pia kuna haja ya kuwa na polisi maalum wa ushirika pamoja na ofisi maalum za mashtaka (DPP) za ushirika ili kudhibiti ubadhirifu na kuhakikisha haki inapatikana kwa wanachama.
Pia ameongeza kuwa, vyama vya ushirika vinazungusha fedha nyingi zenye thamani ya takribani trilioni sita, hivyo kuna kila sababu ya kuweka mifumo madhubuti ya usimamizi ili kuhakikisha fedha hizo zinalindwa na zinawanufaisha wanachama.
Amesema kuwa lengo ni kuhakikisha kunakuwa na uadilifu ndani ya vyama vya ushirika na kuondokana na viongozi wasio waaminifu wanaofanya kazi kwa mazoea, huku akibainisha kuwa baadhi ya vyama tayari vimeanza kuonesha mafanikio makubwa ikiwemo kuanzisha viwanda na kuwanufaisha wanachama wao kwa faida na mikopo yenye riba nafuu.
Awali akizungumza, Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC), Dkt. Benson Ndiege, amesema kuwa kampeni hiyo itadumu kwa miaka mitatu na itakuwa ikifanyiwa tathmini kila mwaka ili kuona mafanikio na changamoto zake.
Aidha amebainisha kuwa, kampeni hiyo itajikita zaidi katika matumizi ya mifumo ya kidijitali, ukaguzi wa mara kwa mara kwenye vyama vya ushirika, pamoja na kuchukua hatua kali kwa watakaobainika kwenda kinyume na taratibu.
Pia ameongeza kuwa kutakuwa na mfumo wa kupokea taarifa kutoka kwa wadau na watoa taarifa (whistleblowers) pamoja na kuanzishwa kwa maafisa uadilifu (integrity officers) ili kusaidia kudhibiti ubadhirifu na kuongeza uaminifu ndani ya vyama vya ushirika.
Aidha, Amebainisha kuwa lengo kuu ni kupunguza ubadhirifu, kuongeza uaminifu na kuhakikisha kuwa vyama vya ushirika vinawanufaisha wanachama wake kwa ufanisi zaidi.





