Na OWM-TAMISEMI, Arusha
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) Bw. Sospeter Mtwale amewataka viongozi wapya waliochaguliwa katika Mkutano Mkuu Maalum wa Uchaguzi wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuhakikisha malengo waliyojiwekea yanafikiwa.
Bw. Mtwale ameyasema hayo leo Aprili 23, 2026 jijini Arusha, baada ya kutangazwa kwa mshindi wa nafasi ya Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa umoja huo, watakaodumu kwa muda wa miaka mitano (5).
Bw. Mtwale amesema ushindi wa viongozi hao ni dhahili kuwa wajumbe wana imani nao hivyo wakatekeleze majukumu yaliyo mbele yao kwa ufanisi na uadilifu.
Katika uchaguzi huo Meya wa Jiji la Mwanza, Mhe. Sima Constantine Sima, ameibuka mshindi kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa ALAT Taifa baada ya kupata kura 273 kati ya kura 339 zilizopigwa.
Mstahiki Meya wa Jiji la Arusha alishika nafasi ya pili kwa kupata kura 45, huku Seif Hassan Daud akishika nafasi ya tatu kwa kura 17.
Kwa upande wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa ALAT Taifa, Agneta Mpangile ameibuka mshindi baada ya kupata kura 189 kati ya kura 337 zilizopigwa. Amefuatiwa na Ali Sadiki Mkaingwa aliyepata kura 118, na Solomon Mabati aliyepata kura 29.
Aidha, uchaguzi kwa nafasi za Wajumbe wa Kamati Tendaji ya ALAT Taifa umefanyika na matokeo yake yatatangazwa mapema kesho.





