
Akizungumza kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Serikali wakati wa uzinduzi wa mradi huo, Dkt. Gunini Kamba iliyofanyika Leo April 24, 2026 jijini Dar es Salaam

…………….
Watoto na vijana 75,500 wanatarajiwa kufanyiwa uchunguzi ili kubaini mapema kama wana ugonjwa wa sikoseli na hivyo kupata huduma muhimu zinazohitajika.
Uchunguzi huo unafanyika kupitia mradi ww wa miaka mitatu wa sikoseli unaotekelezwa katika nchi za Tanzania na Kenya. Kati yao, watoto wachanga ni 45,000, watoto wenye umri chini ya miaka mitano ni 12,500, huku vijana wakiwa 18,000.
Akizungumza kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Serikali wakati wa uzinduzi wa mradi huo, Dkt. Gunini Kamba amesema kuna changamoto ya kuwabaini mapema watoto na vijana wenye ugonjwa wa sikoseli.
Ameongeza kuwa utekelezaji wa mradi huo utawezesha kuwagundua mapema na kuwapatia huduma muhimu wanazohitaji.
Inakadiriwa kuwa asilimia 15 hadi 20 ya Watanzania wanaishi na vinasaba vya sikoseli, huku vifo vya watoto chini ya miaka mitano vinavyotokana na ugonjwa huo vikiwa kati ya asilimia 5 hadi 7.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wataalam Wanaopambana na Sikoseli Tanzania, Dkt. Elisha Osati, amesema mradi huo utasaidia kuwafikia vijana na kubaini hali zao za vinasaba, kwani mtu mwenye vinasaba hawezi kujulikana bila kupimwa.
“Ili mtu apate ugonjwa wa sikoseli, lazima awe na kinasaba kutoka kwa kila mzazi. Hivyo, tunalenga kuwapima vijana na kuwapa elimu sahihi ili wanapoingia kwenye mahusiano waweze kuzingatia hali ya vinasaba vyao na vya wenzao,” amesema Dkt. Osati.
Naye Shujaa wa Sikoseli, Samwel Maingu, amesema aligundulika kuwa na ugonjwa huo akiwa na umri wa miaka 18, na ameishauri jamii kujenga utaratibu wa kupima vinasaba mapema ili kupunguza kasi ya kuenea kwa ugonjwa huo.




