Na Mwandishi Wetu
Baadhi ya abiria na wananchi wameelezea kuridhishwa kwao na uamuzi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuongeza safari za treni za kisasa za SGR kati ya Dar es Salaam na Morogoro kutoka mbili hadi nne kwa siku, wakisema hatua hiyo italeta unafuu mkubwa katika usafiri wa kila siku.
Wakizungumza Aprili 19, 2026 katika maeneo mbalimbali ya mikoa hiyo, wananchi hao walisema ongezeko hilo linakuja wakati muafaka kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya usafiri kati ya Dar es Salaam na Morogoro.
Isakwisa James, mkazi wa Morogoro anayesafiri mara kwa mara kwa kutumia SGR, alisema kuwa hapo awali walikuwa wanakumbana na changamoto ya kupanga safari kutokana na idadi ndogo ya treni.
“Kuongezeka kwa safari hizi ni nafuu kubwa kwetu. Sasa kuna uhakika wa kupata nafasi ya kusafiri bila usumbufu mkubwa,” alisema.
Kwa upande wake, mfanyabiashara Anold Kidwangisa alieleza kuwa hatua hiyo itarahisisha shughuli za kibiashara kati ya mikoa hiyo miwili.
“Hii itasaidia sana wafanyabiashara. Kusafiri kwa uhakika kunapunguza muda wa kusubiri na kuongeza ufanisi katika biashara,” alibainisha.
Naye mwanafunzi wa elimu ya juu, Restituta Komba, alisema hapo awali upatikanaji wa tiketi ulikuwa changamoto hasa nyakati za mwisho wa wiki.
“Sasa tunaweza kupanga safari zetu kwa urahisi zaidi bila presha ya kukosa tiketi,” alisema.
Jijini Dar es Salaam, mkazi wa Yombo Kilakala, Hassan Abukari Mzezele, alisema ongezeko hilo ni faraja kwa familia nyingi zinazotegemea huduma ya treni.
“Huduma imekuwa rafiki zaidi kwa abiria. Tunaweza kuchagua muda unaotufaa bila msongamano mkubwa,” alisema.
Kwa upande mwingine, Mariam Mbeyale alisema uamuzi huo unaonyesha kuwa TRC inazingatia maoni ya wananchi.
“Kadri idadi ya abiria inavyoongezeka, ni muhimu huduma pia iongezwe. Huu ni uamuzi sahihi kabisa,” alisisitiza.
Kwa ujumla, wananchi wengi wanaona ongezeko la safari za SGR kama ishara ya mafanikio ya huduma hiyo na hatua muhimu katika kuboresha usafiri wa uhakika, wa haraka na wenye ufanisi kati ya Dar es Salaam na Morogoro.
Ikumbukwe kuwa Aprili 18, 2026, TRC ilitangaza rasmi kuongeza safari za treni za SGR katika njia ya Dar es Salaam–Morogoro kutoka mbili hadi nne kwa siku ili kukidhi ongezeko la mahitaji ya wasafiri.
