Katibu Mkuu wa Twariqa Taifa, Shehe  Haruna Husein akizungumza kwenye uzinduzi wa sensa hiyo jijini Arusha

………
Na Happy Lazaro, Arusha 
TAASISI YA TWARIQA  makau makuu imezindua rasmi sensa ya waumini wa dini ya Kiislamu lengo kuu likiwa ni kuweza kupata tamwimu sahihi  ya waumini  hao ili kurahisisha utoaji wa huduma za maendeleo kwa  jamii na kwa haraka.
Akizungumza katika hafla hiyo.Hamisi Mkose    kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, Mgeni Rasmi amesema sensa hiyo ni hatua muhimu katika kuhakikisha taasisi za dini zinakuwa na takwimu sahihi zitakazosaidia kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo ya kijamii na kiroho.
Hamis amesema  kuwa sensa ya mwisho ya aina hiyo ilifanyika mwaka 1998, hali inayodhihirisha umuhimu wa zoezi hilo jipya ambalo litaleta taswira halisi ya idadi na mahitaji ya waumini wa Kiislamu kwa sasa.
Aidha  viongozi wa dini na wananchi kwa ujumla wametakiwa  kuimarisha mshikamano, ushirikiano na kulinda amani ya nchi ili kufanikisha maendeleo ya jamii.
Amesema kuwa mafanikio ya maendeleo hayawezi kupatikana bila ushirikiano madhubuti kati ya Serikali na taasisi za dini, akisisitiza kuwa taasisi hizo zina mchango mkubwa katika kujenga maadili, amani na mshikamano wa jamii.
“Serikali inaamini katika umoja na ushirikiano na bila hayo yote hatuwezi kufikia maendeleo bila kushirikiana. Taasisi za dini zina nafasi kubwa ya kujenga jamii yenye maadili na amani,” amesema.
Ameongeza kuwa ingawa Serikali haina dini, wananchi wake wana dini, hivyo ni jukumu la Serikali kuhakikisha kunakuwepo mazingira rafiki kwa taasisi zote za kidini kufanya shughuli zao kwa uhuru na utulivu.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Twariqa Taifa, Shehe  Haruna Husein, amefafanua  kuwa sensa hiyo si ya wanachama bali inalenga kuwatambua waumini wote wa dini ya Kiislamu kwa upana wake.
“Hii si sensa ya wanachama, Uislamu si chama. Tunakusudia kuwafikia Waislamu wote nchi nzima  ili kufahamu mahitaji yao na changamoto zinazowakabili,” amesema Shehe Haruna.
Amefafanua kuwa zoezi hilo litatekelezwa kuanzia ngazi ya mikoa, wilaya hadi vijiji, likihusisha timu maalumu zitakazotambulika rasmi ili kuondoa hofu au mkanganyiko kwa wananchi.
Kwa mujibu wake, sensa hiyo itachukua takribani mwaka mmoja, ikihusisha pia nchi za jirani za Afrika Mashariki, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha mshikamano wa Kiislamu katika ukanda huo.
Naye Kiongozi Mkuu wa Taasisi ya Twariqa Zawiya Kuu Arusha, Shehe Salimu Mbaruku, amesema upatikanaji wa takwimu sahihi ni msingi muhimu wa kupanga mipango endelevu ya maendeleo kwa waumini.
Ameongeza kuwa sensa hiyo itasaidia kubaini mahitaji halisi ya makundi mbalimbali wakiwemo yatima, wajane na vijana, ili kuweka mikakati ya kuwasaidia kwa ufanisi zaidi.
“Hatuwezi kutoa huduma bora bila kujua idadi ya waumini wetu na changamoto zao. Sensa hii itatuonyesha tulipo na wapi tunapaswa kuelekea,” amesema Shehe  Mbaruku.
Amefafanua kuwa zoezi hilo linafanyika kwa ushirikiano wa viongozi wa ngazi zote pamoja na ushiriki wa vijana, jambo linalotarajiwa kuongeza ufanisi wake katika utekelezaji.
Katika tukio la uzinduzi huo, viongozi 12 wa mwanzo walikabidhiwa fomu za ukusanyaji taarifa na kuanza kujaza papo hapo, ikiwa ni ishara ya kuanza rasmi kwa zoezi hilo.
Serikali na viongozi wa dini wamewahimiza waumini kujitokeza kwa wingi kushiriki sensa hiyo na kutoa taarifa sahihi, ili kusaidia kujenga msingi imara wa maendeleo ya taasisi na jamii kwa ujumla.
Aidha Uzinduzi wa sensa hiyo unatazamwa kuwa chachu ya kuimarisha mipango ya maendeleo ya kiroho na kijamii kwa waumini wa Kiislamu nchini na katika ukanda mzima wa Afrika Mashariki.
 Uzinduzi huo ulifanyika katika makao makuu ya taasisi hiyo, Zawiya Kuu jijini Arusha, ukihudhuriwa na waumini kutoka maeneo mbalimbali pamoja na viongozi wa dini na Serikali.