Serikali kupitia Wizara ya Maji imesema inaendelea na programu maalum ya Uhifadhi wa Vyanzo vya Maji inayotekelezwa kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2021 hadi 2035.

Kauli hiyo imetolewa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Kundo Mathew wakati akijibu swalk la mbunge wa viti maalum Katavi Martha Mariki aliyehoji ni upi mkakati wa Serikali katika kulinda Mabonde na Mazingira ili kunusuru uharibifu wa vyanzo vya maji.

Mhandisi Kundo amesema lengo la Mkakati huo ni kulinda mabonde ya maji na mazingira ili kunusuru uharibifu wa vyanzo vya maji Utekelezaji wa programu hiyo unashirikisha Sekta zinazohusiana na maji pamoja na taasisi zake ambapo utekelezaji wake unafanyika kupitia Timu ya Kisekta ya Kitaifa iliyoundwa kwa kujumuisha Sekta za Maji, Kilimo, Mifugo, Maliasili na Mazingira.

“Kupitia Programu hiyo kazi mbalimbali zinatekelezwa ikiwemo kutambua vyanzo vya maji, kuweka mipaka na kuvitangaza vyanzo hivyo kwenye Gazeti la Serikali, kupanda miti rafiki wa maji kwenye vyanzo vya maji; na kufanya kilimo na ufugaji rafiki wa mazingira.

“Hadi sasa jumla ya vyanzo 3,285 vimetambuliwa ambapo kati ya hivyo, 359 vimewekewa mipaka na vyanzo 106 vimetangazwa katika Gazeti la Serikali kuwa maeneo tengefu”amesema Kundo

Hata hivyo ameeleza kuwa jumla ya miti rafiki milioni 6 imepandwa katika vyanzo maji pamoja na kujenga mabirika ya kunywesha mifugo 86 ili kudhibiti uingizaji wa mifugo kwenye maeneo ya vyanzo vya maji na kudhibiti mmomonyoko na uharibifu wa mazingira kwa ujumla.