Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO) imeonyesha kuridhishwa na utekelezaji wa miradi ya umeme kutoka Mkoa wa Tabora hadi Kigoma na kuwahimiza wananchi kuchangamkia fursa za uwepo wa nishati hiyo.
Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa bodi hiyo, Mha. Raymond Mbilinyi, wakati akizungumza na waandishi wa habari Mkoani Kigoma katika ziara yao ya kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na ETDCO.
“Katika miradi yote tuliyoitembelea kuanzia Tabora mpaka Kigoma, tumekuta utekelezaji wake unakwenda vizuri. Ningependa kuwapongeza menejimenti ya ETDCO na wafanyakazi wote kwa kuhakikisha utekelezaji wa miradi unafanyika kama ilivyopangwa,” amesema Mha. Mbilinyi.
Kwa upande wao, wajumbe wa bodi hiyo Adv. Florida Mapunda na CPA Richard Manamba wamefurahishwa na ziara hiyo iliyowawezesha kujionea miradi ya umeme.
“Tumeona jinsi utekelezaji wa miradi ya usafirishaji wa umeme unavyosimamiwa, hasa mradi wa gridi imara kutoka Mkoa wa Tabora hadi Kidahwe, Kigoma, unaotarajiwa kugharimu takribani shilingi bilioni 99 za Kitanzania,” amesema Adv. Mapunda.
CPA. Manamba amesema pia kuna mradi wa usambazaji wa umeme katika Kitongoni, Mkoani Kigoma, wenye thamani ya shilingi bilioni 10.5, unaohusisha ujenzi wa njia za usambazaji na uwekaji wa transfoma kwa ajili ya kusambaza umeme katika vijiji 66.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja Mkuu wa ETDCO, Mhandisi Richard Mwanja, amesema ziara ya bodi hiyo italeta matokeo chanya katika utekelezaji wa miradi hiyo.
“Napenda kuwashukuru wakurugenzi wa bodi kwa kutembelea miradi hii na kutoa mapendekezo kwa ajili ya kuboresha kazi tunazoendelea nazo. Nitoe wito kwa wananchi wa Mkoa wa Kigoma kutumia fursa za kuunganisha umeme,” amesema Mha. Mwanja.
Naye Agenta Kabimba, mkazi wa Kigoma, ameishukuru ETDCO kwa kuwafikishia huduma ya umeme.
“Tunafurahi sana kupata umeme. Zamani tulikuwa tunasikia sehemu nyingine zina umeme na kusikitika kwa kuwa hatukuwa nao. Sasa tunamshukuru Mungu kwa kuwa na sisi tumepata umeme,” amesema Kabimba.
Ziara hiyo imehusisha ukaguzi wa miradi ya Usafirishaji na Usambazaji umeme pamoja maghala ya kuhifadhia vifaa vya ujenzi na vituo vya kupokea na kusambaza umeme kutoka Tabora hadi Kigoma, kwa lengo la kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati ili wananchi waweze kufikiwa na huduma ya umeme na kuchochea ukuwaji wa shughuli za kijamii na uchumi kwanye mikoa hiyo.

