NA DENIS MLOWE IRINGA
SERIKALI imeeleza hatua juu ya ujenzi wa mradi wa soko Machinga Complex Iringa uliopitishwa na Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Iringa mwaka wa fedha 2025/2026 ili kukabiliana na changamoto zinazowakabili wafanyabiashara wadogo na wa kati, hususan uhaba wa maeneo rasmi ya kufanyia biashara.
Akijibu swali la mbunge wa Iringa Mjini Fadhili Ngajilo leo bungeni juu ya hatua zilizofikiwa kuhusu mradi wa ujenzi wa Soko la Machinga katika Manispaa ya Iringa kwa Niaba ya Wizara ya Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi),Mhe. Prof. Riziki Shemdoe Naibu waziri wa wizara hiyo Festo Dugange alisema kuwa mradi huo unatarajiwa kujengwa katika eneo la zamani la stendi ya mabasi lililopo Kata ya Kitanzini, lenye ukubwa wa mita za mraba 6,555, kwa gharama ya shilingi bilioni 4.67. Soko hilo litakuwa na vizimba 800, maduka 150 na migahawa 8, na litahudumia wafanyabiashara 958. Kati yao, wafanyabiashara wadogo watakuwa 800, wa kati 150 na mama na baba lishe 8.
Kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Halmashauri ya Manispaa ya Iringa imetenga shilingi milioni 100 kwa ajili ya maandalizi ya awali ya ujenzi huo.
Akichangia hoja, Mheshimiwa Ngajilo aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wake wa kujenga soko hilo, akibainisha kuwa litawanufaisha kwa kiwango kikubwa wananchi wa Iringa Mjini. Aidha, alihoji iwapo Serikali itawahusisha wafanyabiashara, hususan wamachinga, kabla ya kuanza rasmi ujenzi, pamoja na kutaka kufahamu ni lini ujenzi utaanza.
Akijibu hoja hizo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), alionyesha kuthamini pongezi hizo na akasisitiza kuwa katika miradi yote mikakati, hatua ya kwanza ni ushirikishwaji wa wadau, akiwemo mkurugenzi wa manispaa, baraza la madiwani na wafanyabiashara wa eneo husika.
Alisema Serikali imeendelea kutoa maelekezo kuhakikisha wadau wanafikiwa, wanashirikishwa na wanatoa maoni kabla ya kuanza ujenzi wa soko hilo.
Aidha, Waziri alielekeza Manispaa ya Iringa kuandaa andiko la mradi na kuliwasilisha Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi) kwa ajili ya tathmini na kutafuta fedha za kuunga mkono ujenzi huo, huku akisisitiza umuhimu wa manispaa kuendelea kutenga fedha kila mwaka kupitia mapato yake ya ndani.
Serikali imeahidi kuwa baada ya kukamilika kwa hatua za maandalizi, mradi utaanza kutekelezwa kwa kuzingatia makubaliano na mahitaji ya wafanyabiashara.
