Na Mwandishi Wetu

Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya (DCEA) kutoka Kenya imesema inaendelea na operesheni endelevu za kudhibiti uzalishaji na usambazaji wa dawa za kulevya, ikiwa ni pamoja na kuteketeza mashamba ya bangi na kufuatilia mitandao mipya ya usafirishaji wa dawa hizo haramu.

Akizungumza katika operesheni hiyo,    Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo ametoa wito kwa wananchi kushirikiana kwa karibu na mamlaka husika kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kukomesha biashara hiyo. Alisisitiza kuwa ushirikiano wa jamii ni nguzo muhimu katika vita dhidi ya dawa za kulevya. “Serikali iko makini kuhakikisha inadhibiti kabisa uingiaji wa dawa za kulevya nchini, na tutachukua hatua kali dhidi ya yeyote anayejihusisha na biashara hii,” alisema.

Kwa upande wake, balozi wa shina namba moja katika kitongoji cha Kaole Ufundi, Dominic Masika, ameipongeza Serikali kwa hatua inazoendelea kuchukua katika kukabiliana na tatizo hilo. Alisema tukio lililotokea katika eneo la Kaole, Magambani linaonesha dhamira ya dhati ya Serikali katika kulinda usalama wa wananchi.

Masika aliiomba Serikali kuendeleza operesheni hizo kwa kufanya doria za mara kwa mara na kuwekeza zaidi katika maeneo yenye vichaka ambavyo vinaweza kutumika vibaya kama njia za kupitisha dawa za kulevya. “Naiomba Serikali iendelee kufanya operesheni kama hizi, kwani maeneo haya yanaweza kuwa njia rahisi kwa wahalifu kusafirisha dawa za kulevya,” alisisitiza.

Akizungumzia chanzo cha changamoto hiyo, Masika alieleza kuwa baadhi ya vijana wanajiingiza katika vitendo vya biashara ya dawa za kulevya kutokana na kukosa uelewa sahihi, licha ya malezi wanayopata kutoka kwa wazazi. Alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wazazi, Serikali na viongozi wa mitaa ili kukabiliana kikamilifu na tatizo hilo.