Na Maelezo Zanzibar 05.04.2026
Waziri wa Vijana, Ajira na Uwezeshaji Mhe. Shabaan Ali Othman amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuthamini juhudi za Viongozi na Waasisi wa Mapinduzi kwa kujitoa kwa hali na mali ili kuhakikisha usalama wa nchi.
Ameyasema hayo katika ziara ya kusoma dua katika kaburi la aliyekuwa Brigedia Jenerali Mstaafu Marehemu Yussuf Himid Maftah, katika Msikiti wa Sharifu Msa Mtoni Mkoa wa Mjini Magharibi amesema wiki ya kwanza ya mwezi wa nne imetengwa kwa ajili ya kuwaenzi na kuwakumbuka viongozi walioikomboa nchi.
Amesema wazee hao wamejitoa kwa hali na mali ili kuhakikisha nchi inakuwa na amanj na utulivu, vijana waliopo hivi sasa waweze kuilinda amani na uhuru kwa kujiendeleza kwa lengo la kuleta maendeleo nchini.
Waziri Shaaban amefahamisha kuwa Serikali imefanya jitihada kubwa za kuwaenzi viongozi walioasisi nchi kwa kuleta maendeleo na uhuru ambao wananchi wake wanaendelea kuishi kwa amani na utulivu kitu hicho ni tunu ya kukuza upatikanaji mafanikio katika nchi.
Adha ameeleza kuwa mazuri waliyoaacha viongozi hao wananchi wana wajibu wa kuyatunza na kuendeleza ili yaweze kunufaisha vizazi vijavyo na kukumbuka misingi bora iliyoachwa na waasisi hao.
Amesisitiza maendeleo ya nchi ni msingi imara wa kukuza mafanikio hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kudumisha amani na utulivu iliyopo ili kuendelea kuliweka taifa katika usalama na utulivu.
Kwa upande wake Mjukuu wa Marehemu Yussuf Humid Maftaha Ndugu Abass Himid Yussuf Himid amesema lengo la dua hiyo ni kwaombea viongozi na waasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar ambayo ni zawadi kwa kila maiti ili Allah (S.W) awatilie nuru ndani ya makaburi yao na kumuombea msamaha kusamehewa makosa yao.
Hata hivyo ameeleza kuwa Serikali imeweka utaratibu mzuri wa kuwatembelea na kuwaombea dua waasisi hao licha ya kuwa familia husoma dua hizo lakini Serikali imeonesha kujali na kuthamini mchango wao katika kuipigania na kuigomboa nchi.
Aidha ameiomba Serikali kuendeleza na kukuza zaidi utaratibu huo kwani hiyo huleta faraja kubwa kwa familia na maiti hao kwa kuona bado mchango wao unathaminiwa wa kuipambania nchi dhidi ya udhalimu.
Maadhimisho ya wiki ya kuwaenzi Viongozi wa Kitaifa, Waasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar na Katibu wa Kwanza wa Chama cha Afro Shirazi huadhimishwa kila ifikapo Aprili, 7 ya kila mwaka.

