Na. Meleka Kulwa- Fullshangwe Blog, Dodoma
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Ephatar Mlavi, amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika miundombinu ya barabara na madaraja ili kukuza uchumi wa taifa na kurahisisha usafirishaji.
Aidha, Mhandisi Mlavi amebainisha kuwa hadi kufikia Desemba 2025, asilimia 87 ya barabara za kitaifa ziko katika hali nzuri na ya imara, jambo linaloonyesha jitihada za Serikali katika kulinda uwekezaji uliopo na kuhakikisha usafiri endelevu wa mizigo na abiria.
Akizungumza na waandishi wa habari Machi 30, 2026 jijini Dodoma, amesema kuwa uwekezaji huo umeimarisha kwa kiasi kikubwa kuchochea biashara za ndani na za kikanda.
Aidha, amebainisha kuwa barabara ni mhimili mkuu wa uchumi kwani zaidi ya asilimia 80 ya usafirishaji wa mizigo na abiria hutegemea barabara, hali inayosukuma Serikali kuendelea kuimarisha sekta hiyo.
Pia ameongeza kuwa hadi Desemba 2025, mtandao wa barabara nchini umefikia kilomita 182,164.41, huku TANROADS ikisimamia kilomita 37,734.41 za barabara za kitaifa.
Aidha, amebainisha kuwa miradi ya barabara yenye urefu wa kilomita 5,769.74 inaendelea kutekelezwa, huku miradi mikubwa 79 yenye thamani ya zaidi ya trilioni 6 ikiwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Pia ameongeza kuwa madaraja makubwa nane yamekamilika kujengwa ikiwemo Daraja la J.P. Magufuli na Daraja la Tanzanite, huku mengine 17 yakiendelea kujengwa nchini.
Katika hatua nyingine, amesema kuwa Serikali imeimarisha udhibiti wa uzito wa magari kwa kuongeza mizani na kutumia teknolojia ya kisasa, hatua inayolenga kulinda barabara dhidi ya uharibifu.
Aidha, amebainisha kuwa zaidi ya ajira 16,000 zimezalishwa kupitia miradi ya miundombinu, huku Serikali ikiendelea kuweka mikakati ya kuongeza ushiriki wa wazawa katika miradi hiyo.
Pia ameongeza kuwa licha ya mafanikio hayo, bado kuna changamoto zikiwemo mabadiliko ya tabianchi, ukuaji wa haraka wa miji na kupanda kwa gharama za vifaa vya ujenzi, ambapo Serikali inaendelea kuchukua hatua kukabiliana nazo.

