NA DENIS MLOWE IRINGA
KAMPENI kubwa ya upandaji miti imezinduliwa rasmi katika Kata ya Mshindo, ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Iringa , ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha mazingira na kurejesha historia ya kijani katika maeneo ya makazi.
Uzinduzi huo umefanyika katika eneo la kata hiyo ambapo viongozi, wataalamu wa mazingira na wananchi wamejitokeza kwa wingi kuunga mkono zoezi hilo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi, Meya wa Manispaa ya Iringa, Ibrahim Ngwada, alisema uamuzi wa kufanyika kwa tukio hilo katika Kata ya Mshindo unatokana na historia ndefu ya kata hiyo kuwa na miti mingi ya matunda katika makazi yake.
Alieleza kuwa wakati wa ukuaji wake, karibu kila nyumba katika Mshindo na Miyomboni Kitanzini na maeneo ya jirani ilikuwa na miti ya matunda kama maembe, mipera,, limao pamoja na mikorosho midogo, hali iliyowafanya wakazi kupata matunda kwa urahisi bila kutoka nje ya makazi yao.
Hata hivyo, Meya Ngwada alieleza kuwa kwa sasa nyumba nyingi zimepoteza miti hiyo kutokana na ujenzi wa kisasa na kukua kwa maisha ya wakazi wa kata hiyo. “Leo nimejaribu kukumbuka, nimehesabu nyumba tatu au nne tu ndizo bado zina miti ya zamani. Ni jukumu letu kurejesha utamaduni huu,” alisema.
Alisisitiza kuwa kila nyumba katika Kata ya Mshindo na katika maeneo yote ya Iringa inapaswa kuwa na angalau mti mmoja, iwe ndani ya uzio wa nyumba au nje, ili kuchangia katika kuifanya Iringa kuwa ya kijani na yenye mandhari maridadi.
Alitoa wito kwa wenyeviti wa mitaa na watendaji kuhakikisha miti inayotolewa inasambazwa kwenye kaya zote na kupandwa ipasavyo.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa, Happiness Nnko, alieleza kuwa halmashauri imefanikiwa kuzalisha zaidi ya miche 500,000 ya miti ya kivuli na zaidi ya miche 100,000 ya miti ya matunda kama maembe, mapapai na mipera.
Alisema kuwa lengo kuu ni kuongeza uoto wa kijani, kuboresha lishe kwa wananchi na kuongeza vyanzo vya maji katika maeneo mbalimbali ya manispaa.
Aidha, halmashauri imezalisha kiasi kikubwa cha miche ya miti ya kuhifadhi vyanzo vya maji pamoja na miche ya maua kwa ajili ya kupendezesha mitaa na taasisi.
Katika mpango wa kuongeza miti kwenye taasisi za elimu, zaidi ya miti 250 imepangwa kupandwa katika Shule ya Msingi Mshindo.
Wananchi waliohudhuria hafla hiyo walikabidhiwa miche ya miti ambayo wataipanda katika makazi yao, ikiwa ni sehemu ya ushiriki wao katika kulinda mazingira. Uongozi wa manispaa uliwataka kuhakikisha wanaitunza miti hiyo kwa kufuata maelekezo ya wataalamu.
Mwenyekiti wa mtaa, Zainabu Mpinge, aliwataka wakazi kuitumia vizuri fursa hiyo kwa kupanda na kutunza miti kama wanavyotunza vitu vingine muhimu majumbani kwao, akisisitiza kuwa miti hiyo itakuwa chanzo cha kivuli, matunda na urithi mzuri kwa watoto wao.
Halmashauri imeahidi kuendeleza utoaji na usambazaji wa miche katika kata zote za manispaa, ikiwa ni sehemu ya malengo makubwa ya kuifanya Iringa kuwa mji wenye mazingira bora, salama na yenye mvuto nchini.

