Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za. Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia Miundombinu, Mhandisi Rogatus Mativila, amesema Serikali inaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya uboreshaji wa miundombinu katika Jiji la Dar es Salaam, huku akiwataka wananchi kushiriki kikamilifu katika utunzaji wake ili idumu kwa muda mrefu.

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa miradi ya barabara katika maeneo ya Ubungo na Kinondoni chini ya Mradi wa Uboreshaji wa Jiji la Dar es Salaam (DMDP), Mativila alisema miradi hiyo inazingatia vigezo vya kimazingira ikiwemo udhibiti wa mito na mmomonyoko wa ardhi.

“Tulizingatia masuala ya mazingira, hususan mito, kwa kujenga kingo za mawe kulinda miundombinu isiharibiwe na maji na kuzuia taka zisizibe makaravati,” alisema.

Alibainisha kuwa pamoja na juhudi hizo, bado kuna changamoto ya uchimbaji holela wa mchanga kwenye mito unaofanywa na baadhi ya wananchi, hali inayoweza kuhatarisha uimara wa miundombinu.

“Uchimbaji huo unaweza kufikia hadi kwenye msingi wa makaravati na kusababisha daraja au barabara kuporomoka,” alionya.

Aidha, aliwataka wananchi kuacha kutupa taka ovyo kwenye mifereji na miundombinu ya barabara, akieleza kuwa tabia hiyo husababisha kuziba kwa njia za maji na kuharibu barabara.

Mhandisi Mativila pia alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi za kutafuta fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo, akisema hatua hiyo imeanza kubadilisha maisha ya wananchi kwa kuboresha upatikanaji wa huduma za usafiri.

Katika utekelezaji wa mradi huo, alisema Wilaya ya Ubungo inanufaika na ujenzi wa barabara 23 zenye urefu wa kilomita 52.35, huku mradi mzima wa DMDP katika manispaa tano ukifikia takribani kilomita 250 za barabara.

Kwa upande wa barabara ya Msumi (km 9.9), alisema ujenzi umefikia asilimia 66, huku mkandarasi akiwa nyuma ya muda kutokana na changamoto za uhamishaji wa miundombinu ya DAWASA na TANESCO pamoja na masuala ya fidia.

“Mradi ulitakiwa kufikia asilimia 90 kwa sasa, lakini upo asilimia 66. Mkandarasi ameomba nyongeza ya miezi minne kukamilisha kazi,” alieleza.

Aliongeza kuwa Serikali itaendelea kutafuta rasilimali fedha ili kuboresha mtandao wa barabara, akibainisha kuwa bado sehemu kubwa ya barabara nchini hazina lami.

“Tuna zaidi ya kilomita 148,700 za barabara chini ya TARURA, lakini asilimia 2.6 tu ndizo zenye lami, hivyo bado kuna kazi kubwa mbele yetu,” alisisitiza.