Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Amiri Mkalipa, akizungumza na waumini wa Kiislamu, wakati wa Baraza la Idd El Fitri, kwenye Uwanaj wa Nyamagana, leo.

Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Hasani Kakebe (wa nne kutoka kushoto) akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Amiri Mkalipa (wa tatu kutoka kushoto), na Katibu wa CCM mkoani humu, Omar Mtuwa (wa pili kutoka kushoto), baada ya kumalizika Baraza la Idd El Fitri. Picha na Baltazar Mashaka 

………..

NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA

SERIKALI mkoani Mwanza imesisitiza kuwa itaendelea kushirikiana na waumini wa dini zote bila ubaguzi, kwa lengo la kujenga taifa lenye umoja, upendo, mshikamano na ustawi wa pamoja.

Kauli hiyo ilitolewa Machi 21, 2026 katika Baraza la Idd na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Amri Mkalipa, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, ambapo alieleza dhamira ya serikali katika kuimarisha ushirikiano na taasisi za kidini.

Alisema Mkuu wa Mkoa atahakikisha masuala ya waumini wa Kiislamu yanapatiwa kipaumbele stahiki, bila kuathiri misingi ya serikali isiyo na dini, ili kuchochea maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.

Mkalipa alisema,  serikali imedhamria na itaendelea kushirikiana na waumini wa dini zote katika kudumisha amani, utulivu na mshikamano, na  hali ya usalama mkoani humo inaendelea kuimarika kutokana na ushirikiano huo.

Alimpongeza Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Hasani Kabeke, kwa mchango wake katika kuhubiri na kulinda amani, hali inayochangia kuifanya Mwanza kuwa sehemu salama ya kuishi.

Katika hatua nyingine, Mkalipa alitoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanawapeleka watoto wenye umri chini ya miaka 10 kupata chanjo ya ugonjwa wa kupooza (polio), itakayotolewa kuanzia Machi 24 mwaka huu.

Alisema kuwa, kampeni hiyo inalenga kuimarisha kinga ya watoto dhidi ya maambukizi ya virusi vinavyoshambulia ubongo na uti wa mgongo, ambavyo vinaweza kusababisha ulemavu wa kudumu au hata kifo.

Kwa mujibu wa Mkalipa, chanjo ya polio ni salama na ni muhimu  kuzuia na kutokomeza ugonjwa huo, ambao mara ya mwisho kuripotiwa nchini ilikuwa Julai, 1996.

Alizitaka taasisi za kidini kushirikiana na serikali katika kutoa elimu kwa jamii ili kuhakikisha kampeni hiyo inafanikiwa, huku akisisitiza  ushiriki wa wananchi wote kuwa n muhimu kuhakkisha watoto wanaostahili wanapata chanjo hiyo.

Alieleza kuwa zoezi hilo litafanyika kwa siku nne kuanzia Machi 24 hadi 27, likihusisha utoaji wa chanjo nyumba kwa nyumba, shuleni na katika vituo vya kutolea huduma za afya.

Kwa mujibu wa wtaalamu wa afya, ugonjwa wa polio hauna tiba, hivyo chanjo ndiyo kinga pekee dhidi ya ugonjwa huo, na kuonya jamii kuepuka dhana potofu zinazoeleza kuwa ugonjwa huo husababishwa na imani za kishirikina.

Aidha, hatua ya kuendesha kampeni hiyo imekuja kufuatia kubainika kwa kirusi cha polio katika sampuli za maji machafu mkoani Mwanza, hali inayohitaji kuchukua tahadhari ya haraka ili kulinda afya ya jamii.