Waziri wa Kilimo, Mhe. Japhet Hasunga(wa pili kushoto) akiangalia baadhi ya mashine za kuchambua pamba zinavyofanya kazi, wakati alipotembelea kiwanda cha kuchambua pamba cha Alliance Ginnery kilichopo Kasoli wilayani Bariadi, Mkoani Simiyu Juni 15, 2019.(wa nne kushoto) Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka.
Meneja wa Kiwanda cha kuchambua pamba cha Alliance Ginnery kilichopo Kasoli wilayani Bariadi(kushoto) akitoa maelezo ya aina za mbegu za pamba zinazozalishwa katika kiwanda hicho kwa Waziri wa Kilimo, Mhe. Japhet Hasunga,(wa pili kushoto) na viongozi wengine wa Mkoa wa Simiyu wakati wa ziara yake mkoani Simiyu Juni 15, 2019.
Waziri wa Kilimo, Mhe. Japhet Hasunga(kushoto) akiangali namna taarifa za wakulima zinavyoandikwa mara baada ya pamba yao kupimwa wakati alipotembelea moja ya Chama cha Msingi Cha Ushirika (AMCOS)kilichopo kata ya Luguru wilayani Itilima, wakati wa ziara yake Mkoani Simiyu, Juni 15, 2019
Waziri wa Kilimo, Mhe. Japhet Hasunga akiangalia baadhi ya marobota ya pamba iliyochambuliwa katika kiwanda cha NGS kilichopo Majahida wilayani Bariadi, mara baada ya kutembela kiwanda hicho wakati wa ziara yake Mkoani Simiyu, Juni 15, 2019.
Mkurugenzi wa Kiwanda cha NGS kilichopo Majahida Bariadi ambaye pia ni Mbunge wa Itilima, Mhe. Njalu Silanga(wa tatu kulia) akitoa maelezo kwa Waziri wa Kilimo, Mhe. Japhet Hasunga (wa tatu kulia), na viongozi wengine wa Mkoa wa Simiyu wakati wa ziara ya Waziri huyo mkoani Simiyu Juni 15, 2019.
Baadhi ya viongozi na wataalam wa mkoa wa Simiyu wakimsikiliza Waziri wa Kilimo, Mhe. Japhet Hasunga(hayupo pichani) wakati alipozungumza nao katika Ofisi ya Mkuu wa mkoa kabla ya kuanza ziara yake mkoani humo, Juni 15, 2019.
Mbunge wa Itilima, Mhe. Njalu Silanga akiwasilisha kero za wananchi zinazohusu kilimo kwa Waziri wa Kilimo, Mhe. Japhet Hasunga(kulia) katika Mkutano wa hadhara uliofanyika Katika Kijiji cha Inalo Kata ya Luguru wilayani Itilima, wakati wa ziara ya Waziri huyo mkoani Simiyu Juni 15, 2019
Mjumbe wa NEC kupitia Mkoa wa Simiyu, Mhe. Gungu Silanga akichangia hoja katika kikao cha ndani kati ya Waziri wa Kilimo, Mhe. Japhet Hasunga na viongozi pamoja na watendaji mbalimbali, wakati wa ziara ya Waziri huyo mkoani Simiyu Juni 15, 2019.
******************************
Na Stella Kalinga, Simiyu
Waziri wa Kilimo amewaomba wanunuzi wa pamba waliopewa leseni na Bodi ya pamba wanunue pamba kwa wakulima kwa bei elekezi ya shilingi 1200 kama ilivyopangwa na kukubaliwa katika kikao cha wadau wa pamba mwezi Mei, 2019 jijini Mwanza.
Waziri Hasunga ameyasema hayo Juni 15, 2019 wakati wa ziara yake Mkoani Simiyu wakati alipotembelea viwanda vya kuchambua pamba, vituo vya kununulia pamba na kuzungumza na wananchi kupitia mkutano wa hadhara.
“Naomba nitumie nafasi kuwaomba wanunuzi wa pamba wenye nia njema na nchi hii waliopewa leseni na Bodi ya Pamba waje kununua pamba kwa wakulima, bei elekezi ya mwaka huu ni shilingi 1200”-alisema Waziri Hasunga.
Aidha, Waziri Hasunga amevitaka vyama vya ushirika vya msingi kuzikagua mizani kwani itakapobainika kufanyika uchakachuaji wakati wa kupima hatua kali zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria, huku akiwahakikishia wakulima kuwa changamoto zote zilizobainishwa na wakulima katika msimu wa 2018/2019 zitafanyiwa kazi.
Mkulima wa Pamba kutoka Luguru wilayani Itilima, Bw. Ngusa Lutenganeja ameishauri Serikali kupanga bei ya pamba wakati wa maandalizi ya msimu ili wakulima walime wakiwa wanafahamu bei na maandalizi ya fedha yafanyike mapema wakulima wasikopwe pamba yao.
Kwa upande wake Mnunuzi wa pamba ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Itilima, Mhe. Njalu Silanga amesema imani yake ni kwamba Serikali itasimamia na kuhakikisha pamba ya wakulima inanunuliwa kwa bei elekezi ya shilingi 1200/= na wananchi wanapata fedha zao kwa wakati.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema mkoa wa Simiyu una viwanda vingi vya kuchambua pamba, ambapo ameshauri kuwa ili kuliongezea thamani zao la pamba Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na wadau wengine kuona uwezekano wa kujenga kiwanda cha kutengeneza nguo kwa kuwa uhakika wa soko la bidhaa zitakazotengenezwa upo.
Katibu wa Chama cha Wanunuzi wa pamba nchini (TCA), Bw. Boaz Ogola ametoa wito kwa Wanunuzi wa pamba kuunga mkono juhudi za Serikali katika viwanda kwa kuwekeza kwenye viwanda vya kuongeza thamani ya pamba ili tusitegemee soko nje ambalo linayumba.