Afisa Mradi wa shirika hilo ,Gloria Vicent akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kikao hicho jijini Arusha leo .

Happy Lazaro, Arusha

Arusha. Shirika lisilo la kiserikali la Blue Cross Society of Tanzania limewataka wanahabari na taasisi mbalimbali kuimarisha ushirikiano katika kutoa elimu kinga kwa jamii kuhusu madhara ya matumizi ya dawa za kulevya, pombe na tumbaku, pamoja na uhusiano wake na vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Wito huo umetolewa leo na Afisa Mradi wa shirika hilo ,Gloria Vicent wakati wa kikao cha mafunzo kwa wanahabari kilichofanyika Arusha, kwa lengo la kuongeza uelewa na kuwajengea uwezo wa kuwasilisha taarifa sahihi zitakazosaidia jamii kutambua madhara ya matumizi ya vilevi.

Amesema moja ya changamoto zilizopo ni taarifa zinazotolewa kwa jamii kutobainisha wazi uhusiano uliopo kati ya matumizi ya pombe, dawa za kulevya na tumbaku na matukio mbalimbali ya ukatili, hivyo kuwataka wanahabari kuzingatia ukweli na chanzo cha matukio wanapoyaripoti ili wananchi wapate uelewa sahihi na kufanya maamuzi yenye manufaa kwa maisha yao.

“Wanahabari wanakabiliwa na changamoto ya kupata taarifa sahihi na takwimu kutoka katika taasisi zinazohusika na masuala hayo, hali inayoweza kuathiri uwezo wao wa kueleza ukubwa wa tatizo na kuibua hatua za kukabiliana nalo.”amesema Gloria .

Kutokana na hali hiyo, amezitaka Blue Cross pamoja na taasisi nyingine zenye mamlaka kuimarisha ushirikiano na wanahabari kwa kuwapatia taarifa na takwimu sahihi kwa wakati ili kuongeza ufanisi wa utoaji elimu na uhamasishaji kwa jamii.

Kwa upande wake, Mmmoja wa washiriki katika semina hiyo, John Martin amesema mafunzo hayo yamemwezesha kujifunza mambo mapya kuhusu madhara ya matumizi ya dawa za kulevya, pombe na tumbaku, akibainisha kuwa elimu haina mwisho na semina zinazozingatia hali halisi ya jamii zina umuhimu mkubwa kwa wanahabari.

Amesema kama mwandishi wa habari atatumia kalamu na maarifa aliyoyapata kuelimisha jamii na kuchochea mabadiliko ya tabia, huku akieleza kuwa changamoto nyingine wanazokutana nazo wanahabari ni ugumu wa kupata na kusawazisha taarifa kutoka mamlaka mbalimbali zinazohusika na masuala hayo.

Ameongeza kuwa wanahabari ni daraja linalounganisha jamii na taarifa kutoka katika taasisi mbalimbali, hivyo amezitaka mamlaka husika kutoa ushirikiano kwa wakati wanapohitaji taarifa ili kuwawezesha kutekeleza wajibu wao wa kuhabarisha na kuelimisha umma.