Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Hamdoun Mansoor akiwaonesha ramani Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii eneo la mradi wa upangaji na upimaji ardhi katika manispaa ya Shinyanga jana wakati wa kukagua mradi huo mkoani Shinyanga. Katikati anayeangalia ramani hiyo ni Mwenyekiti wa Kamati Kemilembe Lwota.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kemilembe Lwota akitoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga Geofrey Mwangulumbi (aliyevaa Kaunda suti) wakati Kamati yake ilipokwenda kukagua mradi wa upangaji na upimaji ardhi katika manispaa hiyo jana mkoani Shinyanga.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga Geofrey Mwangulumbi akitoa ufafanua mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu mradi wa Upangaji na upimaji ardhi katika manispaa hiyo wakati kamati hiyo ilipokwenda kukagua maendeleo ya mradi huo jana. Kulia ni Mwenyekiti wa Kamati Kemilembe Lwota.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii wakifuatilia uwasilishwaji taarifa ya mradi wa Upangaji na upimaji ardhi katika Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga jana walipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo mkoani Shinyanga.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, viongozi wa mkoa wa Shinyanga na watendaji wa Wizara ya Ardhi wakimsikiliza Mbunge wa Kaliua Magdalena Sakaya wakati kamati hiyo ilipotembelea mradi wa Kupanga na kupima katika manispaa ya Shinyanga jana. (PICHA NA WIZARA YA ARDHI)
*******************************
Na Munir Shemweta, WANMM SHINYANGA
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Malisili na Utalii imeridhishwa na maendeleo ya mradi wa kupanga, kupima na kumilikisha ardhi katika Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga mkoani Shinyanga.
Mradi huo wa viwanja 320 ni mkopo usio na riba wa shilingi milioni 240 kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga ukiwa na lengo la kuongeza kasi ya upangaji, upimaji na umilikishaji ili kuondoa migogoro ya ardhi.
Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua mradi huo mkoani Shinyanga jana Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kemilembe Lwota alisema kamati yake imeridhishwa na mradi huo na kuuita wa mfano kwa kuwa umetekelezwa kwa asilimia mia moja.
Kwa mujibu wa Kemilembe, kati ya halmashauri 24 zilizopatiwa mkopo wa aina hiyo halmashauri nne zimerejesha fedha zilizokopeshwa kwa asilimia mia moja na baadhi yake zimepata faida kupitia mkopo huo ikiwemo Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga na kuzitaka halmashauri nyingine kwenda kujifunza katika Manispaa hiyo.
‘’Sote tunajua migogoro ya ardhi iliyopo Tanzania na tumekuwa tukihimiza kwa muda mrefu upangaji, upimaji na umilikishaji maeneo ili kuondoa migogoro na nia ya kamati yetu ni kutaka kuona kila kipande cha ardhi kinapimwa’’ alisema Kemilembe
Aliipongeza Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa hatua kubwa ya kutoa fedha za mkopo usio na riba kwa halmashauri ili kuongeza kasi ya upangaji ambapo alitoa wito kwa wananchi kununua maeneo yaliyopimwa na kumilikishwa kwa kuwa hati zake zinaweza kutumika kuchukulia mkopo benki.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alisema pamoja na mamlaka ya upangaji kuwa chini ya halmashauri lakini Wizara yake iliamua kuziwezesha baadhi ya halmashauri kwa kuzipatia mkopo wa fedha usio na riba ili kuongeza kasi ya upangaji, upimaji na umilikishaji maeneo.
Amezitaja halmashauri zilizopatiwa mkopo katika mkoa wa Shinyanga mbali na Manispaa ya Shinyanga kuwa ni halmashauri ya Mji wa Kahama milioni 220 na ile ya Mji wa Msalala milioni 120 ambazo zote zimefanikiwa kurejesha mikopo yake kwa asilimia mia moja
‘’ Lengo la Wizara ya ardhi ni kupanga, kupima na kumilikisha kila kipande cha ardhi nchini na mkopo tunaoutoa sasa kwa baadhi ya halmashauri unatokana na upatikanaji fedha ‘’ alisema Dkt Mabula.
Hata hivyo, Naibu Waziri Mabula alisema, Wizara yake katika siku zijazo ina mpango wa kupima kila kipande cha ardhi kutokana na Benki ya Dunia na ile ya Exim-Korea kuonesha nia ya kusaidia zoezi hilo na kusisitiza kuwa suala hilo litakapofanikiwa migogoro ya ardhi nchini itapungua kama siyo kuisha kabisa.