NA DENIS MLOWE, IRINGA
WANAWAKE wametakiwa kutokata tamaa wanapokutana na changamoto mbalimbali za maisha, bali watumie nguvu ya ndani waliyonayo kujitoa katika hali ngumu na kufikia mafanikio.
Wito huo umetolewa Mtaalam wa Saikolojia Moses Muya wakati wa Kongamano la Wanawake wa Manispaa ya Iringa kuelekea kilele cha Siku ya Wanawake Duniani ambapo mazungumzo yaliyolenga kuwahamasisha wanawake kutambua thamani yao na uwezo wao wa kushinda maumivu ya maisha.
Akizungumza katika mkutano huo Muya aliwahimiza wanawake kukumbuka kuwa changamoto wanazopitia leo hazipaswi kuwazuia kusonga mbele.
Alisema kuwa kila mwanamke ana nguvu ya kipekee inayoweza kumtoa katika giza la huzuni na kumpeleka kwenye mwanga wa mafanikio.
Alisisitiza kuwa wanawake hawapaswi kuruhusu maumivu ya jana kuharibu furaha ya leo, bali wanapaswa kusimama imara, kusonga mbele na kuonesha nuru yao kwa jamii.
Alieleza kuwa mara nyingi watu hukabiliwa na msongo wa mawazo unaotokana na matatizo mbalimbali ya maisha kama vile madeni, migogoro ya kifamilia, changamoto za kulea watoto, pamoja na matatizo ya kazini. Alifananisha hali hiyo na ndoo inayojazwa maji taratibu mpaka kufikia kiwango cha kujaa, akieleza kuwa msongo wa mawazo unapoongezeka bila kupunguzwa huweza kusababisha mtu kubadilika kitabia.
Kwa mujibu wa maelezo yake, baadhi ya watu wanapopatwa na msongo wa mawazo huanza kujitenga na wengine, hubadilisha tabia ya kula kwa kula kupita kiasi au kupunguza ulaji, hali ambayo inaweza kuashiria changamoto ya afya ya akili.
Aliongeza kuwa wengine hutafuta njia za muda mfupi za kupunguza mawazo kama vile unywaji wa pombe au kutafuta burudani zisizosaidia kutatua chanzo cha tatizo.
Alisema njia hizo hufanana na kufungua bomba la juu kwenye ndoo iliyojaa maji, ambapo kwa muda mfupi inaonekana kama maji yanapungua lakini baadaye hurudi tena ndani ya ndoo hivyo alisisitiza umuhimu wa kutafuta suluhisho la kudumu kwa kushughulikia chanzo cha matatizo badala ya kukimbilia njia za muda mfupi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Zaina Mlawa alitumia nafasi hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Samia Suluhu Hassan kwa kuwapa nafasi wanawake katika ngazi za juu katika mikoa mbalimbali kwani unaonesha kuwa wanawake wana uwezo wa kushika nafasi kubwa za uongozi serikalini.
Alisema kuwa uwepo wa wanawake katika nafasi za juu za maamuzi ni ishara ya maendeleo na usawa wa kijinsia, na unatoa motisha kwa wanawake wengine kujituma katika elimu, kazi na uongozi.
Aidha alieleza kuwa mafanikio ya wanawake waliopo kwenye nafasi za uongozi yanapaswa kuwa chachu kwa wanawake wengine kuamini kuwa wanaweza kufikia mafanikio makubwa endapo watatumia vizuri elimu, maarifa na uzoefu wao.
Mlawa alisisitiza kuwa wanawake wanapaswa kuendelea kushirikiana, kusaidiana na kuhamasishana ili kufikia maendeleo ya pamoja katika jamii na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mgeni Rasmi wa Kongamano hilo. Kamishina Msaidizi wa Ardhi mkoa wa Iringa Rehema Kilonzi, amesema wanawake wamepiga hatua kubwa katika kupata nafasi za uongozi na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.
Bi. Kilonzi alisema wiki hii imekuwa muhimu kwa wanawake kujadili mafanikio waliyoyapata pamoja na changamoto zinazohitaji kufanyiwa kazi ili kufikia usawa wa kijinsia.
Alisema maadhimisho hayo yanatokana na maazimio yaliyowekwa baada ya Beijing World Conference on Women, ambayo yalilenga kuimarisha haki na nafasi za wanawake duniani.
Alifafanua kuwa kaulimbiu ya mwaka huu inasisitiza kuwa Haki na Usawa kwa Wanawake na wasichana ni msingi muhimu wa kufikia maendeleo jumuishi ifikapo mwaka 2050. Kwa mujibu wake, hatua mbalimbali zimeanza kuonekana nchini ambapo wanawake wengi zaidi wameanza kupata nafasi za uongozi katika sekta mbalimbali.
Bi. Kilonzi pia aliipongeza serikali kwa kuendelea kuweka mazingira rafiki yanayowezesha wanawake kupata elimu, ajira na nafasi za uongozi huku akitoa mfano wa hatua ya kihistoria ya nchi kupata Rais mwanamke kupitia Samia Suluhu Hassan, jambo alilosema limeongeza hamasa kwa wanawake wengi kuamini kuwa wanaweza kushika nafasi za juu za uongozi.
Aidha, alieleza kuwa hata katika sekta ya ardhi kumekuwa na mabadiliko makubwa ya kisheria yaliyosaidia kusogeza huduma karibu na wananchi.

