Na John Walter – Manyara

Wazazi wamekumbushwa kuwa makini na watoto wao hasa wale wanaoishi karibu na makorongo makubwa au maeneo yenye mikondo ya maji, wakati mvua zikiendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini.

Wito huo umetolewa na Inspekta wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Manyara, Gilbert Mushi, alipokuwa akizungumza na kituo hiki kuhusu tahadhari za kuchukua kipindi hiki cha mvua.

Mushi amesema ni muhimu kwa wazazi kufuatilia kwa karibu watoto wao, hususan wanapokwenda na kurudi shule, ili kuepuka hatari ya kusombwa na maji au kuanguka katika makorongo na maeneo yenye mafuriko.

Aidha, amewakumbusha madereva kuongeza umakini barabarani kwa kuendesha kwa tahadhari zaidi kipindi hiki cha mvua, ili kuepusha ajali zinazoweza kusababishwa na utelezi wa barabara pamoja na mwonekano hafifu.

Katika hatua nyingine, Jeshi hilo limewakumbusha wananchi kupiga namba ya dharura 114 pindi ajali au majanga yanapotokea katika maeneo yao, ili kurahisisha juhudi za uokoaji na kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.

Amesema ushirikiano wa wananchi na vyombo vya uokoaji ni muhimu katika kuokoa maisha na mali za watu wakati wa majanga mbalimbali.