Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Kusimamia Uuzaji Nyumba 4000 katika eneo la Vingunguti Dar es Salaam pamoja na Kampuni ya PMM 2001 Ltd inayonunua nyumba hizo walipokutana katika ofisi za Wizara jijini Dodoma mwishoni mwa wiki wakati wa kutafuta muafaka wa ununuzi nyumba hizo. Wa pili kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Segerea Bona Kamoli, wa kwanza kulia ni Mwenyekiti wa Kamati Ramadhani Pepo, wa pili kulia ni Mkurugenzi wa Fedha na Utumishi wa Kampuni ya PMM 2001 Ltd Damian Kanuti na wa tatu kushoto ni Katibu wa Kamati Ibrahim Mkumbi.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimsikiliza Katibu wa Kamati ya Kusimamia Uuzaji Nyumba 4000 katika eneo la Vingunguti Dar es Salaam Ramadhani Pepo alipokutana na Kampuni ya PMM 2001 Ltd inayonunua nyumba hizo pamoja na Kamati jijini Dodoma mwishoni mwa wiki wakati wa kutafuta muafaka wa ununuzi nyumba hizo. Wa pili kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Segerea Bona Kamoli, wa pili kulia ni Mkurugenzi wa Fedha na Utumishi wa Kampuni ya PMM 2001 Ltd Damian Kanuti na wa tatu kushoto ni Katibu wa Kamati Ibrahim Mkumbi (PICHA NA WIZARA YA ARDHI)
******************************
Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameagiza kupitiwa upya Mkataba wa Mauziano ya nyumba baina ya Kampuni ya PMM 2001 Ltd na Wamiliki wa nyumba 4000 wakazi wa Vingunguti jijini Dar es Salaam.
Uamuzi huo unafuatiwa kutozingatiwa kwa masharti ya Mkataba ulioingiwa awali ambao umeonekana kuwa na mapungufu mengi ya kisheria na hivyo kusababisha kampuni ya PMM 2001 Ltd kushindwa kuwalipa Wamiliki wa nyumba katika eneo la Vingunguti kwa takriban miezi tisa kama walivyokubaliana jambo lililozua taharuki kwa wamiliki wa nyumba hizo.
Dkt Mabula alitoa agizo hilo mwishoni mwa wiki baada ya kukutana na pande zote mbili za Kamati inayosimamia makubaliano ya uuzaji nyumba 4000 katika mitaa minne ya Vingunguti ambayo ni Mnyamani, Mtambani, Mtakuja na Faru, kampuni ya PMM 2001 Ltd na Mbunge wa Jimbo la Segerea Bona Kamoli katika ofisi za Wizara jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisema, baada ya kupitia Mkataba wa mauziano ya nyumba katika eneo la Vingunguti kati ya Kampuni ya PMM 2001 Ltd na Wamiliki wa nyumba katika eneo la Vingunguti wamebaini mkataba kutofuata taratibu za kisheria na kubainisha kuwa wamiliki ambao hawajalipwa fedha yoyote hawabanwi na mkataba huo na wanaweza kuzifanyia shughuli yoyote nyumba zao.
Alisema, kwa zile nyumba themanini (80) ambazo kampuni ya PMM 2001 Ltd ilizinunua kwa wamiliki katika eneo hilo, Wizara yake itatuma timu maalum kufuatilia iwapo Kampuni hiyo imefuata taratibu zote za mauziano ikiwemo kutoa kodi ya serikali na kuongeza kwa kuitaka kuhakikisha inakamilisha taratibu za kumilikishwa nyumba hizo..
Akigeukia suala la Wamiliki wa nyumba 17 ambao kampuni hiyo imewalipa shilingi milioni 35 kwa kila mmoja kama fedha za awali, Naibu Waziri wa Ardhi aliagiza hatua za kisheria zifuate kwa kuwa Mkataba wa Mauziano hauoneshi kiasi kilichobaki baada ya kutolewa cha awali sambamba na muda wa ukamilishaji malipo jambo lililosababisha Wamiliki kufuatilia kwa muda mrefu bila mafanikio.
Kwa mujibu wa Dkt Mabula, ilichofanya kampuni ya PMM 2001 Ltd kwa Wamiliki ni udanganyifu unaoweza kutoa mwanya mkubwa kupoteza haki yao na kusisitiza kuwa Serikali ya awamu ya tano haiko tayari kuona wananchi wanapata tabu kufuatilia haki zao na kuiagiza kampuni hiyo kuwaeleza Wamiliki itawalipa lini kiasi kilichobaki ili kuondoa mkanganyiko.
Hata hivyo, Dkt Mabula alisema, atamuagiza Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Dar es Salaam kuzungumza na wananchi wanaouza nyumba kwa kampuni hiyo na yeye mwenyewe atakupokuwa mkoani humo katika ziara yake atazungumza na wakazi hao wa Vingunguti kuhusiana na sakata hilo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Fedha na Utumishi wa Kapmuni ya PMM 2001 LTD Damian Kanuti alijitetea kwa kueleza kuwa kampuni yake ilishindwa kutekeleza makubaliano ya ununuzi wa nyumba katika mitaa ya Vingunguti kutokana na kuchelewa kupata mkopo ilioutarajiwa kutoka Benki ya TIB na kubainisha kuwa pamoja na sakata hilo lakini kampuni yake ilishalipa kiasi cha bilioni 1.7 ikiwa ni malipo ya nyumba 80 na fedha ya awali kwa Wamiliki 17.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kusimamia Uuzaji nyumba 4000 katika eneo la Vingunguti Ramadhani Pepo ameilalamikia kapuni ya PMM 2001 Ltd kwa kutoonyesha ushirikiano kwa kamati wakati wa zoezi hilo jambo alilolieleza kuwa limesababisha Kamati kufikisha malalmiko kwa Mbunge wa Jimbo la Segerea Bona Kamoli na hatimaye kwa Naibu Waziri wa Arhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula kwa lengo la kupatiwa ufumbuzi
Pepo alisema, kutokana na Kampuni ya PMM 2001 Ltd kushindwa kutekeleza makubaliano yaliyokuwa yatekelezwe Septemba 2018 wamechoka kufuatilia suala hilo na wanachotaka kwa sasa ni wao waliolipwa fedha za awali kukamilishiwa kiasi kilichopaki na hawako tayari kuendelea na zoezi hilo tena kwa kuwa kampuni hiyo imeshindwa kuonesha ushirikiano.
Mbunge wa jimbo la Segerea Bonna Kamoli ameitaka kampuni ya PMM 2001 Ltd kueleza bayana kiasi cha fedha kilichobaki kwa wamiliki wa nyumba 17 zitalipwa lini lakini Mkurugenzi wa Fedha na Utumishi wa PMM 2001 Ltd Kanuti alishindwa kutoa jibu na kutaka kampuni yake kupewa muda kulifanyia kazi suala hilo.