
Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega (wapili kushoto) akikata utepe kama ishara ya uzinduzi wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), wengine ni Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Balozi, Mhandisi Aisha Amour, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TBA, Dkt. Laurean J. Ndumbaro, Mtendaji Mkuu wa TBA na Katibu wa Bodi hiyo, Arch. Daud Kondoro katika hafla fupi iliyofanyika Machi 2, 2026 katika Ofisi za TBA, jijini Dar es Salaam. (PICHA NA NOEL RUKANUGA)

Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega (kushoto) akimpongeza Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TBA, Dkt. Laurean J. Ndumbaro (katikati) baada ya kumkabidhi vitendea kazi.

Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega (kushoto) akimkabidhi vitendea kazi Mtendaji Mkuu wa TBA na Katibu wa Bodi hiyo, Arch. Daud Kondoro (kulia)
Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega akiwakabidhi vitendea kazi wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA)
Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega akizungumza wakati akizinduaBodi ya Ushauri ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA)
Mtendaji Mkuu wa TBA na Katibu wa Bodi ya Ushauri TBA , Arch. Daud Kondoro akizungumza katika uzinduzi wa Bodi hiyo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TBA, Dkt. Laurean J. Ndumbaro akizungumza katika uzinduzi wa Bodi hiyo.
…………………..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega, amezindua Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) na kuitaka kufanya kazi kwa uwazi na ufanisi ili kuboresha utendaji wa taasisi hiyo. Huku akisisitiza umuhimu wa kujenga nyumba za gharama nafuu zitakazowafikia wananchi wa kipato cha chini, pamoja na kufikia malengo ya Serikali ya kujenga nyumba 4,500 kati ya 50,000 ifikapo mwaka 2050.
Akizungumza leo, Machi 2, 2026, jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Bodi hiyo, Mhe. Ulega amesema Tanzania bado ina tatizo kubwa la makazi, na kuhimiza Bodi hiyo kuliangalia suala hilo kwa mapana yake ili kuleta tija kwa Taifa.
Mhe. Ulega ameongeza kuwa ni muhimu kwa Bodi kushirikiana kwa karibu na Wizara katika utekelezaji wa majukumu yake, ikiwemo kutoa taarifa za utekelezaji ili kuwezesha upatikanaji wa maamuzi na miongozo stahiki.
Pia amesema wakati umefika kwa TBA kuweka mazingira rafiki yatakayovutia wawekezaji, hususan kutoka sekta binafsi, ili waweze kuwekeza bila vikwazo visivyo vya lazima.
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TBA, Dkt. Laurean J. Ndumbaro, ametoa shukrani kwa kuaminiwa kuiongoza Bodi hiyo, na kuahidi kusimamia majukumu yake kwa ufanisi ili kuhakikisha TBA inasonga mbele na kufikia malengo yake.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TBA na Katibu wa Bodi hiyo, Arch. Daud Kondoro, amesema taasisi hiyo inaendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi, ikiwemo kusimamia na kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi.
Amefafanua kuwa TBA inaendelea kutoa huduma za ushauri wa ujenzi pamoja na kuendeleza maeneo 149 ya wakala. Aidha, amesema katika utekelezaji wa majukumu yao wamefanikiwa kupata hati safi ya hesabu na kuboresha maslahi ya watumishi.
Miongoni mwa wajumbe katika bodi hiyo mpya ni pamoja na Pendo Mwakisese, Awadhi Abdallah, Dkt. Kimata Malekela, QS. Mwanahamisi Omary, Benno Sanga.
Ni bodi ya sita ya TBA, inayotarajiwa kuleta mageuzi chanya na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
