Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inashiriki Mkutano wa 25 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Nchi zilizopo Mwambao wa Bahari ya Hindi (Indian Ocean Rim Association – IORA), unaofanyika jijini New Delhi, India Novemba 25-27, 2026.
Balozi wa Tanzania nchini India Mheshimiwa Anisa Mbega, anaongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo ambao utawakutanisha Mawaziri wa Mambo ya Nje na Makatibu Wakuu kutoka Nchi Wanachama wa IORA kujadili masuala ya kikanda na kimataifa yanayohusu ulinzi na usalama baharini, maendeleo endelevu na ustawi wa Ukanda wa Bahari ya Hindi.
Mkutano huo umetanguliwa na Kikao cha 29 cha Kamati ya Makatibu Wakuu wa Nchi Wanachama (29th Committee of Senior Officials – CSO) unaofanyika Novemba 25-26, 2026 na utafuatiwa na Mkutano wa 25 wa Baraza la Mawaziri (25th Coucil of Ministers – COM) utakaofanyika Novemba 27,2026.
Mkutano huo unafanyika chini ya uenyekiti wa India kwa kipindi cha 2025–2027, chini ya kauli mbiu isemayo “Ubunifu, Uwazi, Ustahimilivu na Uwezo wa Kukabiliana na Mabadiliko katika Ukanda wa Bahari ya Hindi.”(Innovation, Openness, Resilience and Adaptability in the Indian Ocean Region”, ambayo inasisitiza umuhimu wa ubunifu, uwazi, ustahimilivu na uwezo wa kukabiliana na mabadiliko katika eneo la Bahari ya Hindi.
Mkutano huo unajadili masuala ya kuimarisha usalama na usafiri baharini, biashara na uwekezaji, uchumi wa buluu, usimamizi endelevu wa rasilimali za bahari, pamoja na kuhakikisha mtiririko mzuri wa biashara na minyororo ya ugavi.
Mkutano pia unatoa fursa kwa nchi wanachama kutathmini utekelezaji wa maamuzi yaliyopita, kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kidiplomasia na kuweka mikakati ya pamoja ya kukabiliana na changamoto zinazozikabili nchi za ukanda huo.
IORA yenye Nchi Wanachama 23 pamoja na Nchi 12 Washirika wa Majadiliano (Dialogue Partners) ilianzishwa 1997 kwa lengo la kukuza ushirikiano wa kikanda katika maeneo kipaumbele na masuala mtambuka , ikiwemo biashara na uwekezaji, Ulinzi na usalama baharini, uvuvi, usimamizi wa majanga, Elimu,sayansi na teknolojia,Uinuaji Wanawake kiuchumi na uchumi wa buluu.

