Mwakilishi wa FAO Dkt.Tipo Nyabenyi akizungumza kwenye uzinduzi huo jijini Arusha.

Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tuliesther Mwambapa akizungumza kwenye uzinduzi huo mkoani Arusha.

……….
Na Happy Lazaro, Arusha
Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limeanza jitihada za kuziwezesha taasisi mbalimbali za fedha nchini Tanzania ili kuwawezesha wazalishaji wadogo wa mazao ya misitu na kilimo kupitia hifadhi ya mazingira, ambao kwa muda mrefu walikuwa hawakopesheki, ili waendelee kutunza na kuhifadhi mazingira.
Akizungumza katika uzinduzi wa mfuko wa kuwezesha wazalishaji wa mazao ya misitu na kilimo, Dkt. Joseph Otieno kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii amesema mfuko huo utasaidia kuziba pengo la kifedha lililokuwepo kwa miaka mingi.
Dkt.Otieno amesema kuwa,hapo awali wazalishaji wa misitu walishindwa kupata mikopo kutokana na ukweli kwamba uwekezaji wa misitu huchukua muda mrefu kukua na kuleta faida.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa FAO Dkt.Tipo Nyabenyi, amesema kuwa mradi huo unalenga kuunganisha sekta ya fedha na juhudi za uhifadhi wa mazingira, ili kuhakikisha wakulima na wazalishaji wa misitu wanapata mitaji rafiki itakayowasaidia kuendeleza shughuli zao kwa njia endelevu.
Dkt. Tipo amesema mpango huo si wa ruzuku bali unalenga kuhamasisha uwekezaji wenye tija na kujenga uendelevu tofauti na mipango ya awali.
Naye Mratibu wa Mtandao wa Wakulima na Wafugaji mkoa wa Arusha (Mviwarusha),Richard Masandika, amesema kuwa ,kuwepo kwa mradi wa mfuko huo utasaidia kuwezesha vikundi vya fedha ambavyo vitasaidia moja kwa moja kwenye urejezaji wa maeneo ya mazingira vijijini .
Amesema kuwa mradi huo unatarajia kurejeza mazingira kama hekari milioni mia moja Afrika ambapo kwa hapa Arusha na karatu lengo ni kurejeza hekari 70,000.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tuliesther Mwambapa, ameishukuru shirika la chakula Duniani kwa kuichagua CRDB FOUNDATION kwenye mpango huo na kusema kwa kushirikiana na FAO, mpango huo utawezesha wakulima na wazalishaji wadogo kupata mikopo yenye masharti nafuu pamoja na mafunzo ya kibiashara.
Zaidi ya shilingi milioni 200 zimetolewa katika awamu ya kwanza ya mfuko huo, ambapo fedha hizo zitatolewa kwa wazalishaji wa misitu na wakulima wadogo. Mbali na mikopo, wanufaika watapatiwa pia elimu na mafunzo maalum yanayolenga kuwajengea uwezo katika kilimo na uhifadhi endelevu wa mazingira.
Aidha Mfuko huo unatarajiwa kuwa chachu ya mabadiliko kwa wazalishaji wa mazao ya misitu na kilimo, kwa kuwawezesha kupata mitaji na kuchangia ukuaji wa sekta hiyo nchini.
