Na Ashrack Miraji,Fullshangwe Media
Mbunge wa Jimbo la Vunjo, Enock Koola, amekutana na maimamu wa misikiti 57 iliyopo ndani ya jimbo hilo na kufanya kikao maalum cha mashauriano pamoja na dua.
Akizungumza katika kikao hicho, Mheshimiwa Mbunge aliwashukuru viongozi wa dini kwa ushirikiano waliouonesha kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu, pamoja na kuendelea kuwa karibu naye katika utekelezaji wa majukumu yake ya kuwatumikia wananchi.
“Naomba nitumie nafasi hii kuwashukuru sana viongozi wangu kwa dua na ushirikiano mliouonesha kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu, pamoja na kuendelea kuwa karibu nami wakati wote ninapowahitaji. Naombeni mniombee ili niendelee kuwatumikia wananchi wa Jimbo la Vunjo na Watanzania kwa ujumla,” alisema.
Kikao hicho kilifanyika katika eneo la Msikiti wa Himo Mjini na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini na Serikali, akiwemo Sheikh wa Mkoa wa Kilimanjaro, Kadhi wa Mkoa pamoja na Makadhi wa Wilaya, viongozi wa Wilaya na Mwenyekiti wa Baraza la Waislamu Moshi Vijijini, Hussein Jamal, pamoja na Katibu wake.
Katika kuadhimisha kipindi hiki cha Mfungo Mtukufu wa Ramadhani, Mheshimiwa Mbunge alikabidhi sadaka ya tende kwa misikiti yote 57 ya Jimbo la Vunjo, akieleza kuwa ni ishara ya mshikamano, upendo na kuthamini mchango wa taasisi za dini katika kujenga maadili na amani ndani ya jamii.
Aidha, alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya viongozi wa dini na viongozi wa Serikali ni nguzo muhimu katika kuimarisha ustawi wa wananchi, akiahidi kuendelea kushirikiana nao katika masuala ya kijamii na maendeleo.
Kwa upande wao, maimamu wa misikiti hiyo walimshukuru Mbunge kwa kuthamini mchango wa viongozi wa dini katika jamii na kumtaka aendelee kusimama imara katika kuwatumikia wananchi bila kuchoka.
Viongozi hao wa dini walimfanyia dua maalumu wakimuombea afya njema, ulinzi na hekima ili aendelee kutekeleza majukumu yake kwa uadilifu, uwajibikaji na kujituma kwa manufaa ya Jimbo la Vunjo na Taifa kwa ujumla.

