NA DENIS MLOWE IRINGA 

JUMUIYA ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Iringa Vijijini imeanza ukurasa mpya wa kujitegemea kiuchumi baada ya kukabidhiwa shilingi milioni 2 kutoka kwa Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa, Arif Abri, kwa ajili ya kuanzisha mchakato wa ununuzi wa maeneo ya miradi.

Msaada huo umetolewa tarehe 28 Februari 2026 katika kikao cha kawaida cha Baraza la Wazazi, hatua ambayo imeelezwa kuwa ishara ya mwamko mpya wa maendeleo ndani ya jumuiya hiyo.

Akitoa taarifa ya shughuli za jumuiya, Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Iringa Vijijini, Anitha Magelanga, amesema changamoto ya kutokuwa na miradi endelevu imekuwa ikikwamisha ufanisi wa shughuli za kila siku pamoja na kupunguza ushiriki wa wanachama, hususan wale waliokosa nafasi za uongozi katika ngazi za udiwani na ubunge.

Amefafanua kuwa mipango ya jumuiya hiyo kwa sasa inalenga kujenga nyumba ya mtumishi wa wazazi wilaya, kuanzisha miradi ya muda mfupi na mrefu itakayoongeza mapato, pamoja na kuimarisha elimu ya maadili na malezi kwa jamii.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya hiyo, Mario Kihongo, amemshukuru Arif Abri kwa kuendelea kuiunga mkono jumuiya, akisema msaada huo umeleta hamasa mpya kwa wanachama na kuwa chachu ya kusukuma gurudumu la maendeleo.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu wa CCM Wilaya ya Iringa Vijijini, Sophia Nyalusi ambaye pia ni Katibu wa UWT wilaya, amewapongeza wanachama kwa kazi waliyoifanya wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, akisema mchango wao umechangia ushindi wa chama katika nafasi za Rais, wabunge na madiwani.

Naye Arif Abri ambaye alikuwa mgeni rasmi aliwasisitiza wajumbe wa Baraza la Wazazi, na kuwataka kuongeza juhudi katika malezi ya vijana kwa kuwajenga katika misingi ya uzalendo, amani na uadilifu. 

Alisema kuwa katika mazingira ya sasa ambapo dunia inabadilika kwa kasi, jukumu kubwa liko kwetu wazazi kuhakikisha vijana wetu hawapotei katika vishawishi, mmomonyoko wa maadili, na vitendo vinavyochafua taswira ya taifa.

Aidha alisema ni lazima tusimame kidete kupiga vita rushwa, ubadhirifu, ukatili dhidi ya wanawake na watoto, na tabia za ulevi kupita kiasi.

Chama chetu kinahitaji wanachama safi, viongozi safi, na jamii safi.

Amesema jumuiya ya wazazi ndiyo nguzo ya maadili ndani ya chama na taifa, hivyo ni muhimu ikasimamia kwa uthabiti miradi itakayozinduliwa ili iweze kuzaa matunda.

Aidha Alifu Abri aliwaomba jumuiya ya wazazi kuhamasisha wanachama kujiunga kwenye vikundi vya uzalishaji, kwenye mikopo ya Halmashauri, na kwenye fursa zinazoletwa na serikali.

“Tusikubali wanachama wetu kuwa maskini wakati serikali ya chama chetu imefungua milango ya mikopo, mafunzo, na miradi ya kuinua kipato” Alisema

Kupokea kwa mchango huo na kuanza kwa mchakato wa ununuzi wa maeneo ya miradi kumetajwa kuwa mwanzo wa safari mpya ya mageuzi ya kiuchumi ndani ya Jumuiya ya Wazazi CCM Iringa Vijijini, ikiwa na dhamira ya kuijenga jumuiya imara, yenye mchango mkubwa katika kulea jamii na kuchochea maendeleo ya wilaya kwa ujumla.